Popular services

WADIWANI NA WATENDAJI WA BARAZA LA MANISPAA KASKAZINI A WAENDELEA NA ZIARA WAPIGA HATUA KUJIFUNZA UTAWALA BORA DODOMA.

 

Na Nishan Khamis, Dodoma
Waheshimiwa madiwani pamoja na watendaji wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A wanaendelea na ziara yao ya mafunzo katika Jiji la Dodoma, yenye lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya kiutendaji ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, ujumbe huo unapata fursa ya kujifunza kwa kina kuhusu mbinu bora za usafi wa mazingira na usimamizi wa taka ngumu, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji, uchakataji na utupaji salama wa taka. Mafunzo haya yanawalenga kuwajengea uwezo viongozi hao katika kuimarisha mikakati ya usafi na usarifishaji wa taka katika maeneo yao, sambamba na kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.

Aidha, wajumbe wa ziara hiyo wanajifunza namna bora ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kutumia mifumo ya kisasa na mikakati madhubuti inayolenga kuongeza ufanisi na uwazi. Kupitia mafunzo haya, wanatarajia kuongeza uwezo wa halmashauri katika kukusanya mapato yatakayochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Vilevile, masuala ya utoaji wa huduma za kijamii yamepewa kipaumbele katika ziara hiyo, ambapo wajumbe wanajifunza namna bora ya kuboresha sekta kama afya, elimu na huduma nyingine muhimu kwa wananchi. Lengo kuu ni kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa ubora na kwa wakati huku zikizingatia viwango vinavyotakiwa.

Ziara hii pia inaakisi jitihada kubwa zinazofanywa na madiwani pamoja na Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A katika kuimarisha utendaji kazi na kuwajibika kwa wananchi wao.

Kupitia dhamira yao ya kujifunza na kuboresha mifumo ya usimamizi, viongozi hao wanaonyesha nia thabiti ya kuleta mabadiliko chanya, kuongeza ufanisi wa huduma na kuchochea maendeleo endelevu kwa jamii wanayoihudumia, wakitumia uzoefu wanaoupata katika Jiji la Dodoma.