Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Mhe. Riziki Daniel Yussuf, amewataka masheha kutoa elimu kwa jamii kuhusu vitendo vya watu kunyang’anywa nyeti zao, suala ambalo limeanza kujitokeza kwa kasi katika wilaya hiyo.
Akizungumza na masheha wa wilaya hiyo leo katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkokotoni, amesema kuwa takribani matukio manne yameripotiwa tangu jana, jambo linaloweza kuleta taswira mbaya katika jamii.
Amesisitiza umuhimu wa masheha kushirikiana na viongozi wa dini pamoja na wadau wengine katika kutoa elimu kwa wananchi ili kukomesha vitendo hivyo.
Aidha, ameitaka jamii, hususan vijana, kuepuka kujichukulia sheria mkononi pale matukio kama hayo yanapotokea, badala yake kutoa taarifa kwa vyombo husika ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Vilevile, amesema tangu alipokabidhiwa madaraka, ameomba ushirikiano kutoka kwa masheha ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi na mshikamano kwa lengo la kuleta maendeleo ya wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao, masheha wameahidi kutekeleza maagizo yote waliyopewa na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkuu wa Wilaya, huku wakitoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria pale matukio mbalimbali yanapotokea.
