Popular services

WIZARA YA AFYA YASISITIZA MIKAKATI MADHUBUTI KUDHIBITI MALARIA ZANZIBAR

 

Na Nishan Khamis, Zanzibar
Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Uhamasishaji Jamii cha Kupambana na Malaria Zanzibar, imewataka wananchi kushirikiana katika kuandaa na kutekeleza mikakati madhubuti ya kudhibiti ugonjwa huo, hasa katika kipindi hiki cha mvua.

Akizungumza na wahudumu wa afya ngazi ya jamii pamoja na wahamasishaji kutoka Wilaya ya Kaskazini A (Mkoa wa Kaskazini Unguja) na Wilaya za Kati na Kusini (Mkoa wa Kusini Unguja), katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Tumekuja, Wilaya ya Mjini, Unguja, Afisa Uhamasishaji wa Programu ya Kutokomeza Malaria Zanzibar, Bishara Hemed, amesema makundi hatarishi zaidi ni pamoja na wajenzi, wavuvi, waendesha bodaboda, walinzi, wanafunzi na mama lishe.

Amesema makundi hayo huathirika zaidi kutokana na mazingira yasiyo salama pamoja na uhalisia wa kazi zao, ambapo wengi hufanya kazi nyakati za usiku na mara nyingi hawavai mavazi marefu yanayoweza kuwakinga dhidi ya mbu.

Aidha, ameeleza kuwa ugonjwa wa malaria husababishwa na vimelea aina ya Plasmodium, vinavyoenezwa na mbu jike aina ya Anopheles wanaozaliana katika maji yaliyotuama kama vile madimbwi, mahodhi, pamoja na maji yanayohifadhiwa majumbani kwenye ndoo na chupa zisizofunikwa. Ameongeza kuwa mbu hao wanaweza pia kuzaliana katika kiwango kidogo cha maji yaliyotuama kwenye vitu kama vifuniko vya chupa, vifuu vya nazi, mifuko na hata majani.

Kwa mujibu wa Afisa huyo, dalili za malaria ni pamoja na maumivu ya kichwa, maumivu ya viungo, kutapika, kuharisha na kupoteza hamu ya kula. Ameonya kuwa kupuuza dalili za awali kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa damu, kuathirika kwa viungo muhimu vya mwili kama figo na ini, kuharibika kwa mimba na hata kifo.

Vilevile, amebainisha kuwa uingiaji na utokaji wa watu kupitia bandari zisizo rasmi, mabadiliko ya tabianchi pamoja na uwepo wa mazingira hatarishi, ni miongoni mwa sababu zinazoendelea kuchangia kuwepo kwa malaria Zanzibar. Hata hivyo, amesisitiza kuwa licha ya kupungua kwa maambukizi, bado juhudi za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa kabisa.

Ameongeza kuwa utunzaji sahihi wa taka ngumu, kuzitupa katika maeneo yaliyotengwa, kufukia madimbwi ya maji, kufyeka vichaka pamoja na matumizi sahihi ya vyandarua, ni miongoni mwa mikakati muhimu ya kudhibiti na hatimaye kuutokomeza ugonjwa wa malaria.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuweka miundombinu imara ya huduma za afya, jambo linalotoa matumaini ya kutokomeza malaria kwa wakati uliopangwa.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza elimu waliyoipata na kuahidi kuwa mabalozi wazuri katika jamii zao kwa kushirikiana kikamilifu katika mapambano dhidi ya Malaria.