Popular services

 Na,Nishan khamis, Wilaya ya Kaskazini A.

14,April 2026.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Mhe. Riziki Daniel Yussuf, amewataka watendaji wa wilaya hiyo kuzingatia nidhamu, ushirikiano pamoja na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuendeleza maendeleo ya wilaya hiyo.

Mhe. Riziki Daniel Yussuf amesema hayo leo wakati akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika katika ofisi za wilaya Gamba, Wilaya ya Kaskazini A, kufuatia uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais tarehe 10 Aprili 2026.

Katika hotuba yake, ametoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo ya uongozi.

Amesema ataendelea kuitumia nafasi hiyo kuhakikisha analeta maendeleo endelevu katika Wilaya ya Kaskazini A na Taifa kwa ujumla.

Aidha, amesisitiza kuwa ataongoza kwa misingi ya uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi, huku akiahidi kushirikiana kwa karibu na watendaji wote wa serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Ndugu Rashid Simai Msaraka, amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kulitumikia taifa kwa takribani miaka sita.

Amesema katika kipindi chote cha uongozi wake, amefanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa wafanyakazi wa wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi kwa ujumla. Aidha, amewataka watendaji hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mkuu mpya wa Wilaya ili kuhakikisha maendeleo yanaendelea kupatikana.

Ndugu Msaraka pia ameahidi kuwa yupo tayari kutoa ushauri na ushirikiano wakati wowote utakapohitajika katika kuendeleza jitihada za maendeleo ya wilaya hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Mkurugenzi wa Halmashauri, Hassan Thabit, ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mkuu mpya wa Wilaya kama walivyofanya kwa uongozi uliopita.