MWANDISHI: NishanKhamis, Moga.
Wakazi wa kijiji cha Moga Mwembe Mkali, kilichopo wadi ya Kidombo, jimbo la Mkwajuni, wilaya ya Kaskazini A, wamelalamikia hali mbaya ya barabara katika kijiji hicho, wakisema ni changamoto kubwa inayosababisha usumbufu kwa wananchi, hususan wagonjwa, watu wenye ulemavu na wanawake wajawazito wanapohitaji kufika hospitali.
Wakizungumza leo na waandishi wa habari kijijini hapo, wakazi hao wamesema tatizo hilo limekuwepo kwa takribani miaka 45, hali inayozidi kuwa mbaya hasa wakati wa msimu wa mvua. Wameeleza kuwa hali hiyo inaathiri zaidi wazee, wagonjwa na wanawake, hivyo kuiomba serikali kuchukua hatua za haraka kulitatua tatizo hilo.
Kwa upande wake, Diwani wa wadi ya Gamba ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa la wilaya hiyo, Mheshimiwa Nyange Kher Ali, amesema kuwa suala la barabara ya Moga Mwembe Mkali ni la kipaumbele na linatambulika serikalini. Ameeleza kuwa barabara hiyo ipo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na tayari changamoto hiyo imewasilishwa katika wizara husika kwa ajili ya hatua zaidi.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuwa na subira wakati taratibu za utekelezaji wa mradi huo zikiendelea, huku akiahidi kuwa Baraza la Manispaa litachukua hatua za muda mfupi, ikiwemo kuweka kifusi ili kupunguza adha hiyo wakati wakisubiri ujenzi wa barabara ya kudumu.
Aidha, amewapongeza viongozi wa juu wa nchi kwa juhudi zao katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar na taifa kwa ujumla.
