Popular services

DIWANI KHAMIS PICHI ATOA MIFUKO 10 YA SARUJI KUWAWEZESHA VIJANA UJENZI WA BANDA LA UJASIRIAMALI CHAANI

 

Mwandishi: Nishan Khamis, Chaani
Diwani wa Wadi ya Chaani, Mheshimiwa Khamis Pichi, leo ametekeleza ahadi yake kwa vijana wa UVCCM pamoja na Baraza la Vijana wa Shehia ya Chaani Kubwa kwa kuwapatia mifuko kumi (10) ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa banda lao la ujasiriamali katika shehia hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika Tawi la CCM Chaani Kubwa, Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini A, Mheshimiwa Khamis amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya juhudi zake za kuendelea kuwawezesha vijana kiuchumi.

Ameeleza kuwa kuwawezesha vijana ni njia muhimu ya kuwaunga mkono viongozi wakuu wa nchi katika azma ya kuhakikisha vijana wanajiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Aidha, diwani huyo amesisitiza kuwa ataendelea kushirikiana bega kwa bega na vijana hao katika nyanja mbalimbali za maendeleo, sambamba na viongozi wa jimbo hilo kwa ujumla. Pia amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani, utulivu na mshikamano ndani ya jamii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mifuko hiyo ya saruji imegharimu kiasi cha shilingi laki mbili (200,000).

Katika hatua nyingine, Diwani wa Kuteuliwa kutoka Ofisi ya Rais, Idara Maalum za SMZ, Mheshimiwa Haji Ali, naye ameahidi kuchangia mifuko mingine kumi (10) ya saruji ili kuunga mkono na kuhamasisha ujenzi huo wa banda la ujasiriamali.

Kwa upande wao, vijana wa UVCCM na Baraza la Vijana wa Shehia ya Chaani Kubwa wamemshukuru Mheshimiwa Khamis Pichi kwa kutekeleza ahadi yake, wakisema msaada huo ni chachu kubwa ya kuendeleza ndoto zao za kujiajiri.

Wamesema kuwa watautumia msaada huo kwa uadilifu na kwa malengo yaliyokusudiwa, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wao katika kuleta maendeleo.

Vijana hao pia wameeleza kuwa hatua hiyo imewapa hamasa mpya ya kujituma zaidi katika shughuli za kiuchumi pamoja na kuimarisha mshikamano wao, wakisisitiza kuwa wataendelea kuwa walinzi wa amani na utulivu katika eneo lao.