Popular services

 Tarehe, 10 April 2026.

Nishan Khamis, Mkwajuni.

Uimarishwaji wa miundombinu bora ya elimu nchini unaofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Hussein Ali Mwinyi, umetajwa kuwa ni chachu ya mabadiliko makubwa ya ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne katika Wilaya ya Kaskazini A.

Kauli hiyo imetolewa na Diwani wa eneo hilo, Ali Chumu Haji, wakati akizungumza na wazazi, walimu, wanafunzi pamoja na kamati ya skuli ya Sekondari Mkwajuni, katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2025. Tukio hilo limefanyika katika Skuli ya Sekondari Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A.

Amesema juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa madarasa, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuimarisha walimu, zimekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ari ya wanafunzi kusoma kwa bidii na hatimaye kufanya vizuri katika mitihani yao.

Aidha, Diwani huyo ametoa pongezi za dhati kwa marais wote wa nchi kwa juhudi zao katika kuimarisha sekta ya elimu, akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu katika elimu. Katika kuunga mkono jitihada hizo, amechangia shilingi milioni moja pamoja na polo  kumi za  mchele kwa ajili ya kambi ya wanafunzi wa kidato cha nne wanaojiandaa na mitihani yao.

Sambamba na hilo, amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kutumia vyema muda wao ili waweze kufikia malengo yao ya kitaaluma. Pia ameitaka kamati ya skuli kushughulikia changamoto zinazoikabili skuli hiyo ikiwemo uhaba wa maji safi kupitia ujenzi wa kisima pamoja na uimarishaji wa miundombinu ya msikiti kwa ajili ya mahitaji ya kiroho ya wanafunzi.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Mkwajuni, Mustafa Makame Hamad, amesema hali ya ufaulu imeongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka 2025, ambapo zaidi ya wanafunzi 38 wamefanikiwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wazazi na wanafunzi, pamoja na uwepo wa mazingira bora ya kujifunzia. Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna changamoto chache ikiwemo uhaba wa baadhi ya vifaa vya maabara na miundombinu ya maji, ambazo zinahitaji juhudi za pamoja kuzitatua.

Nao baadhi ya wanafunzi wa skuli hiyo wameeleza kufurahishwa na matokeo yao, wakisema juhudi za walimu pamoja na msaada kutoka kwa wazazi zimekuwa chachu ya mafanikio yao. Wameahidi kuendelea kusoma kwa bidii zaidi ili kufikia ndoto zao na kuwa wataalamu watakaosaidia kuijenga jamii na taifa kwa ujumla.