Popular services

DIWANI KIPANGE ATATUA CHANGAMOTO YA MAJI NA UMEME KATIKA KITUO CHA AFYA MKOKOTONI

 DIWANI KIPANGE ATATUA CHANGAMOTO YA MAJI NA UMEME KATIKA KITUO CHA AFYA MKOKOTONI

Tarehe: 7 April 2026
Mwandishi: Nishan Khamis
Diwani wa Wadi ya Kipange, Jimbo la Tumbatu, Khamis Kombo Khamis, ametatua changamoto ya miundombinu ya maji na umeme katika Kituo cha Afya Mkokotoni, hatua ambayo imepokelewa kwa furaha na wananchi pamoja na watumishi wa afya katika eneo hilo.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, diwani huyo amesema hatua hiyo ni sehemu ya wajibu wake katika kuwatumikia wananchi na kuhakikisha wanapata huduma bora za kijamii. Ameeleza kuwa juhudi hizo pia ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na viongozi wa kitaifa, akisisitiza kuwa maendeleo ya wananchi yanahitaji mshikamano wa pamoja.

Ameongeza kuwa ataendelea kushirikiana bega kwa bega na jamii pamoja na viongozi wa jimbo hilo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, hususan katika sekta za afya, elimu na miundombinu.

Diwani huyo amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo umetokana na ziara yake maalum ya kutembelea Kituo cha Afya Mkokotoni, ambapo alibaini uwepo wa changamoto kubwa ya maji na umeme iliyokuwa ikiathiri utoaji wa huduma.

Amesema zaidi ya shilingi laki tisa zimetumika kufanikisha upatikanaji wa huduma hizo muhimu, hatua ambayo sasa imeimarisha mazingira ya utoaji huduma katika kituo hicho.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini, akieleza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Mkokotoni, Makame Juma Sheha, amesema kuwa kwa ushirikiano wa karibu na diwani pamoja na viongozi wengine wa jimbo hilo, wamejipanga kikamilifu kuwatumikia wananchi kwa hali na mali. Ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi na jamii.

Sheha huyo amewasisitiza wananchi kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho, akionya kuwa uharibifu wa mali za umma unarudisha nyuma juhudi za maendeleo.

Kwa upande wao, wafanyakazi wa Kituo cha Afya Mkokotoni wamesema walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya huduma ya maji na umeme kwa muda mrefu, hali iliyokuwa ikiathiri utoaji wa huduma hasa kwa kina mama wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.

Wamesema wakati mwingine walilazimika kutumia njia mbadala zisizo salama, jambo lililokuwa likihatarisha afya za wagonjwa na watumishi. Hivyo, wametoa pongezi za dhati kwa diwani kwa hatua yake ya haraka na ya kizalendo ya kutatua changamoto hiyo.

Wananchi wa eneo hilo pia wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema imeleta matumaini mapya ya upatikanaji wa huduma bora za afya na kuahidi kushirikiana na viongozi katika kulinda na kuendeleza miundombinu iliyowekwa.