Popular services

MHE. MARYAM SAID KHAMIS AWAPATIA MIAMVULI WAJASIRIAMALI WANAWAKE KUSINI PEMBA, AAHIDI KUENDELEA KUWAINUA KIUCHUMI

 

Na Nishan Khamis, Pemba
Mheshimiwa Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba na Mbunge wa Kuteuliwa kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mheshimiwa Maryam Said Khamis, ameendelea kuonesha dhamira yake ya dhati katika kuwawezesha wanawake kwa kutoa msaada wa miamvuli kwa wajasiriamali wanawake wa Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa msaada huo, Mheshimiwa Maryam amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya harakati zake za kuwasaidia wanawake wajasiriamali wadogo wadogo kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo athari za jua kali na mvua zinazoweza kuathiri biashara zao.

Ameeleza kuwa kuwawezesha wanawake ni njia muhimu ya kuimarisha uchumi wa familia na jamii kwa ujumla, huku akiahidi kuendelea kushirikiana nao pamoja na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kufanyia biashara zao.

Aidha, amesisitiza kuwa ataendelea kuwa karibu na wanawake hao na kusikiliza changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu, sambamba na kuhamasisha maendeleo endelevu ya wanawake katika wilaya hiyo na Mkoa wa Kusini Pemba kwa ujumla.

Kwa upande wao, wanawake wajasiriamali walionufaika na msaada huo wameeleza furaha na shukrani zao kwa Mheshimiwa Maryam Said Khamis, wakisema kuwa msaada huo umekuja kwa wakati muafaka na utawasaidia kuimarisha shughuli zao za biashara.

Wamesema kuwa miamvuli hiyo itawalinda dhidi ya hali mbaya ya hewa na hivyo kuongeza ufanisi katika kazi zao za kila siku. Pia wameahidi kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuongeza juhudi katika biashara zao ili kujiletea maendeleo na kusaidia familia zao.

Wanawake hao pia wamempongeza Mheshimiwa Maryam kwa juhudi zake za dhati za kuwajali na kuwaunga mkono wanawake, wakiahidi kuendelea kumuunga mkono katika jitihada zake za kuleta maendeleo katika jamii.