Na Nishan Khamis, Kaskazini Unguja
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kushirikiana na Wasaidizi wa Sheria kutoka Shirika la NAPAC, wamewahimiza wananchi hususan vijana na wanafunzi kujiepusha na vishawishi vyovyote vinavyoweza kupelekea vitendo vya udhalilishaji hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Eid-al-Adha.
Kauli hiyo imetolewa na Inspekta Salum Khamis machano Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Kaskazini Unguja – Mahonda, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo (RPC), wakati wa mazungumzo na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mapinduzi Chaani.
Amesema kipindi cha sikukuu mara nyingi huambatana na ushawishi mkubwa, hususan kwa vijana, hivyo kuna umuhimu mkubwa kwao kujiepusha na mazingira yanayoweza kuwaweka hatarini kufanyiwa vitendo hivyo. Aliongeza kuwa athari za udhalilishaji ni pamoja na kupata maradhi, mimba zisizotarajiwa, msongo wa mawazo, ulemavu, na hata vifo.
Aidha, Inspekta Salum alibainisha kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja lipo imara kuhakikisha usalama na amani vinaendelea kutawala katika kipindi hicho, na akawasihi wanafunzi kuripoti mara moja pale wanapobaini au kushuhudia vitendo vya aina hiyo ili kusaidia kudhibiti janga hilo.
Kwa upande wake, Rashd Haji Khamis (Kunguni) kutoka shirika la International Peace Information, aliwataka vijana kuwa waangalifu na kujitenga na ushawishi wowote unaoweza kusababisha ndoto zao kuvunjika. Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza muda na juhudi katika masomo kama njia pekee ya kufanikisha malengo ya maisha.
Naye Bi Hadia Ali Makame kutoka NAPAC aliwasihi wanafunzi na wananchi kuacha masihara dhidi ya suala la udhalilishaji, akisema kuwa hali hiyo inavunja ndoto nyingi za vijana, hususan watoto wa kike. Alihimiza nidhamu kwa walimu, wazazi na jamii, pamoja na kuvaa mavazi ya staha kipindi cha sikukuu ili kujikinga na vishawishi vya udhalilishaji.
Wanafunzi wa shule hiyo waliwapongeza wageni hao kwa nasaha walizotoa na kuahidi kuzizingatia ili kuweza kutimiza malengo yao kwa ajili ya maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla


