Zanzibar.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imetakiwa kufanya juhudi za kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya habari hasa kipindi cha uchaguzi mkuu ili kuhakikisha vyombo vya habari vinapata uhuru wa kufanya kazi zao bila vikwazo na kwa amani.
Wito huo ulitolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Mwinyimvua Nzukwi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Abdala Abdul Rahman, katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani yaliyofanyika ukumbi wa Sanaa Rahaleo, Mjini Unguja.
Nzukwi alisisitiza kwamba kukusanya na kutoa taarifa ni haki ya msingi na ya kisheria kwa wanahabari, hivyo serikali ina wajibu wa kuwalinda ili waendelee kufikisha taarifa kwa jamii kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Nzukwi aliongeza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kufuata maadili ya kazi zao, hasa katika kuripoti matukio ya uchaguzi, ili kuepuka kusababisha vurugu na maafa kwa taifa.
Alihimiza kuwa uwajibikaji katika tasnia ya habari utasaidia kudumisha amani na utulivu wa kisiasa nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhan, alisema kuwa Wizara ya Habari inaendelea kufanya marekebisho ya sheria ya habari na kwamba hivi karibuni sheria hiyo itakuwa imetekelezwa kikamilifu.
Ramadhan alifafanua kuwa, ili kuimarisha mazingira ya kazi ya waandishi wa habari, Wizara husika inatarajia kuzindua sera ya habari ya Zanzibar ya mwaka 2024 ambayo itawawezesha waandishi kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Mkurugenzi huyo pia alieleza kuwa Idara ya Habari Maelezo inaendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari kwa awamu mbalimbali ili kuwasaidia kuimarisha uwezo wao katika kutoa taarifa zenye usahihi.
Alisema kuwa moja ya vipengele muhimu vitakavyofundishwa ni matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili ili kuepuka makosa ya kiuwandishi yanayochafua hadhi ya vyombo vya habari.
Naye mwandishi wa habari mkongwe, Salim Said, alisema kuwa uhuru wa habari ni muhimu kwa maendeleo ya taifa na inapaswa kuhakikisha haki ya kujieleza inatambulika na kutekelezwa kwa vitendo.
Alisisitiza kuwa, ili waandishi wa habari wafanye kazi zao kwa uhuru, sheria ya habari inapaswa kupitishwa ili kurekebisha changamoto zinazoikumba sekta hiyo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA) na mjumbe wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA- ZNZ), Imane Duwe, alisisitiza kuwa Tume ya Uchaguzi inapaswa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili waweze kuelewa sheria za uchaguzi na namna ya kuripoti matukio hayo bila kuvunja sheria.
Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Mei 3, kwa upande wa Zanzibar, maadhimisho ya mwaka 2025 yalifanyika Mei 17 yakiwa na kauli mbiu "Sheria nzuri ya habari ni chachu ya uchaguzi ulio huru na wa haki", chini ya uratibu wa Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO).



