Popular services

RC MATTAR AHIMIZA WANANCHI KUJITOKEZA KUUPOKEA MWENGE WA UHURU 2025


Na: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, amewahimiza wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake huko Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Mhe. Mattar alisema mkoa wa Kaskazini Unguja unatarajia kuupokea Mwenge wa Uhuru tarehe 19 mwezi huu kutoka Mkoa wa Kusini Unguja. Mwenge huo utakimbizwa katika Wilaya ya Kaskazini ‘B’ siku hiyo na kukesha huko, kisha kuendelea kukimbizwa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ tarehe 20.

Amesema jumla ya miradi saba (7) itatembelewa, ambapo miradi minne (4) itawekwa mawe ya msingi, miwili (2) itakaguliwa, na mradi mmoja (1) utazinduliwa rasmi. Miradi hiyo inahusisha sekta za elimu, afya, kilimo, maji, na barabara. Vilevile, programu sita (6) za mafunzo kwa vijana zitafanyika kuhusu masuala ya uchaguzi, afya na nishati.

RC Mattar ameeleza kuwa jumla ya gharama ya utekelezaji wa miradi hiyo, ikiwemo  sekta binafsi, ni zaidi ya Shilingi Bilioni 123.57 za Kitanzania.

Ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru ni kichocheo kikubwa cha maendeleo. Aidha, amewakumbusha wananchi kulipa tukio hilo uzito unaostahiki.

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni: "Shiriki Uchaguzi kwa Amani na Utulivu."