Popular services

BARAZA LA MADIWANI WILAYA YA KASKAZINI ‘A’ UNGUJA LAFUNGA VIKAO VYA MWAKA 2020–2025 – DC MSARAKA ATOA NENO KWA WAFANYAKAZI WA MANISPAA


Na,Nishan khamis, Kaskazini Unguja. 

Baraza la Madiwani Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja leo limefunga rasmi vikao vya mwaka 2020–2025 katika kikao kilichoongozwa na Mstahiki Meya wa Baraza hilo, Mhe. Machano Fadhil Machano (Babla). Kikao hicho pia kilipitia bajeti ya miezi sita ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akifungua kikao hicho, Meya Babla alitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kasi kubwa ya mabadiliko ya maendeleo katika wilaya hiyo. Aidha, aliwashukuru madiwani wenzake, Chama Cha Mapinduzi, pamoja na viongozi mbalimbali kwa ushirikiano wao katika kipindi chote cha uongozi.

Meya alibainisha kuwa kufungwa kwa kikao hicho haina maana kwamba shughuli za maendeleo zimekoma, bali madiwani wataendelea kutekeleza majukumu yao hadi pale baraza litakapovunjwa rasmi na waziri husika. Hivyo, aliwataka viongozi na wananchi kuendelea kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mhe. Rashid Msaraka, alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi alizotoa wakati wa kampeni za mwaka 2020, na kwa kuendeleza utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Alisema kuwa rais amekuwa kinara wa kuchochea maendeleo nchini.

Mhe. Msaraka pia aliwapongeza madiwani kwa kumudu changamoto mbalimbali katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wao, akisisitiza kuwa walitimiza jukumu lao la kumsaidia rais katika kuwahudumia wananchi. Alitoa wito wa kushirikiana, kusameheana, na kuweka mbele maslahi ya wananchi katika kuendeleza maendeleo ya wilaya.

Vilevile, alitoa wito kwa wafanyakazi wa Baraza na Manispaa kufanya kazi kwa weledi, ubunifu, na uzalendo. Alisisitiza umuhimu wa kumuunga mkono Mkurugenzi mpya wa Manispaa kwa lengo la kuimarisha mapato, usafi, na kubuni miradi ya maendeleo.

Kwa upande wao, madiwani walimshukuru Mwenyezi Mungu na kumpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kuwapa hamasa na mazingira bora ya kutekeleza shughuli za maendeleo katika wadi zao. Pia walitoa shukrani kwa wafanyakazi wa Baraza la Manispaa, Chama Cha Mapinduzi, viongozi wa serikali na wadau mbalimbali waliowasaidia katika kipindi chote cha uongozi wao. Walieleza nia ya kuendelea kushirikiana kwa ajili ya maendeleo zaidi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na madiwani wote wa wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya, makatibu tawala, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, vyombo vya ulinzi na usalama, makatibu na wenyeviti wa CCM, Katibu wa Baraza la Vijana wa wilaya hiyo pamoja na wafanyakazi wa Baraza la Manispaa.