Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja imewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa tija kwa kuandika taarifa mbalimbali za maendeleo ya mkoa huo pamoja na kuibua changamoto za kijamii na kiutendaji, ili kuimarisha maendeleo ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Mattar Zahor Masoud, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake mkokotoni wilaya ya kaskazini A Unguja kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na mahusiano mazuri kati ya ofisi yake na vyombo vya habari katika kutoa taarifa kwa umma.
Mhe. Mattar amesema, kuanzia sasa utaratibu huo wa kukutana na waandishi wa habari utafanyika kila mwisho wa mwezi, ambapo atatoa taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo na pia kutoa fursa kwa vyombo vya habari kueleza changamoto zinazowakabili wananchi.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika mkoa huo, hivyo ni muhimu kwa waandishi kuonesha mafanikio hayo kwa jamii, hususan katika kipindi hiki cha miaka mitano ambacho kimeshuhudia maboresho katika sekta mbalimbali.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, pamoja na utaratibu wa kukutana na viongozi wa serikali na wananchi, uwepo wa mkutano na waandishi wa habari kila mwezi utasaidia wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu maendeleo na mikakati ya serikali katika mkoa huo.
Ameongeza kuwa, mkoa umeandaa mpango maalum wa kusaidia wananchi katika masuala ya kijamii na kiuchumi kupitia makundi mbalimbali, ikiwa ni juhudi za kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Mhe. Mattar pia amewasihi viongozi na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari, huku akiwasisitiza waandishi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na misingi ya taaluma yao kwa manufaa ya mkoa na taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari wa Mkoa huo, Nishan Khamis, amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuanzisha utaratibu huo, akieleza kuwa utarahisisha kazi zao na kuongeza ufanisi katika kuhabarisha umma.
Naye, Mkurugenzi wa Redio Tumbatu FM, Vuai Juma, amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa kwa waandishi wa habari ndani na nje ya mkoa huo kupata taarifa za maendeleo na changamoto, na hivyo kusaidia katika kuibua sauti za jamii kwa ajili ya ustawi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
