Popular services

SKULI YA MKWAJUNI YATIMIZA MIAKA 100,BABLA AHAMASISHA USHIRIKIANO WA WAZAZI NA WALIMU KATIKA MAHAFALI YA KIDATO CHA SITA 2025 ILI KUINUA UFAULU WA WANAFUNZI.


Na: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja.

Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Machano Fadhil Machano maarufu kama Babla, ametoa wito kwa wazazi, walezi na walimu wa Skuli ya Sekondari Mkwajuni kushirikiana kwa karibu ili kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa skuli hiyo.

Babla alitoa wito huo wakati akihutubia mahafali ya Kidato cha Sita yaliyofanyika skuli hapo, yakihusisha walimu, wazazi, na wanafunzi wa Wilaya ya Kaskazini A.

Amesema kuwa serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi imeweka kipaumbele kikubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu katika wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuunga mkono juhudi hizo kwa kushirikiana katika kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kwa maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla.

Aidha, amewahimiza wahitimu kuendelea na elimu ya juu ili kuendana na ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi. Vilevile, aliwataka vijana na jamii kwa ujumla kudumisha amani hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Afisa Elimu wa Wilaya hiyo, Juma Mwadin, alisema kuwa mahafali hayo ni ya kihistoria kwa kuwa ni miongoni mwa matunda ya juhudi za muda mrefu za kuimarisha elimu ya sekondari ya juu katika skuli hiyo.

Alimpongeza Rais Dk. Mwinyi pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa uboreshaji wa miundombinu ya elimu, na kueleza kuwa wanafunzi wameweza kufanya mitihani katika mazingira bora, hali inayotarajiwa kuleta ufaulu mzuri.

Aidha, alishukuru ushirikiano wa walimu, wazazi, na kamati ya skuli kwa kuweka mikakati ya maendeleo ya elimu ndani ya skuli hiyo na wilaya kwa ujumla.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu, mwanafunzi Asia Ali Musa alisema Skuli ya Sekondari Mkwajuni ni miongoni mwa skuli kongwe, kwani ilianzishwa mwaka 1925, na sasa imetimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.

Alibainisha kuwa kwa muda mrefu skuli hiyo ilikuwa ikifundisha hadi Kidato cha Nne pekee, lakini kutokana na jitihada za viongozi wazalendo, mwaka 2011 skuli ilianzisha Kidato cha Tano na Sita, ikiwa ni ya kwanza kufanya hivyo katika mkoa huo.

Aliongeza kuwa mahafali haya ni ya pili kufanyika katika historia ya skuli hiyo, ambapo mahafali ya kwanza yalifanyika mwaka 2016. Mwaka huu, jumla ya wanafunzi 47, wakiwemo wanaume 11 na wanawake 36, wamehitimu Kidato cha Sita.

Asia pia alieleza baadhi ya changamoto zinazowakabili, zikiwemo upungufu wa walimu wa somo la Jiografia kwa Kidato cha Tano na Sita, ushirikiano mdogo wa baadhi ya wazazi katika michango ya kambi, na ukosefu wa eneo rasmi kwa ajili ya kambi za masomo. Aliomba changamoto hizo zitatuliwe ili kuimarisha mazingira ya kujifunza.

Kwa upande wao, baadhi ya wazazi walioshiriki mahafali hayo walitoa ahadi ya kuendeleza ushirikiano na walimu wa skuli hiyo ili kuongeza mafanikio ya kielimu kwa vijana. Waliwatunuku pongezi Rais Dk. Hussein Mwinyi, Wizara ya Elimu, na wadau mbalimbali kwa juhudi zao za kuboresha elimu katika skuli hiyo.