Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), leo imeendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wakazi wa kijiji cha Kigongoni kupitia kliniki ya msaada wa sheria (Legal Aid Clinic).
Huduma hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa LEAP II (Legal Empowerment and Access to Justice Program) unaofadhiliwa na UNDP, ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi kupata haki zao kupitia elimu ya kisheria.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kigongoni kwa niaba ya Mkurugenzi wa NAPAC, Afisa Mfuatiliaji na Tathmini Bi Hadia Ali Makame alisema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kutoa huduma za bure za kisheria kwa wakazi wa wilaya hiyo, hali ambayo imewanufaisha wengi katika kutatua changamoto zao za kisheria.
“Taasisi yetu inalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu haki na sheria katika nyanja mbalimbali ili waweze kujua namna ya kuzifikia haki zao za msingi kwa maendeleo ya jamii,” alisema Bi Hadia.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa Kigongoni na wilaya kwa ujumla kufika katika ofisi za NAPAC ili kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali za kisheria na kutumia fursa za msaada unaotolewa.
Naye Afisa Mfuatiliaji na Tathmini wa NAPAC, Khamis Kombo Ali alisema maendeleo yanayoonekana kijijini hapo ni matokeo ya juhudi za wasaidizi wa sheria wanaotoa elimu kwa jamii, na kwamba wataendelea kutoa huduma hizo kwa lengo la kuleta maendeleo chanya zaidi.
Kwa upande wao, wananchi wa Kigongoni walimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuimarisha miundombinu, hasa ujenzi wa barabara katika kijiji hicho, wakisema kuwa ni tukio la kihistoria katika maisha yao.
Pia, walitoa pongezi kwa NAPAC kwa juhudi zake za uhamasishaji na kusaidia kutatua matatizo ya kisheria yanayowakabili, ikiwemo ukosefu wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto, vijana na watu wazima, upungufu wa huduma katika kituo cha afya, pamoja na tatizo sugu la utoro kwa wanafunzi wa skuli na madrasa.
Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wananchi, Afisa Usajili wa Vizazi na Vifo wa wilaya hiyo, Haji Ali Shamte, alisema ofisi yao inaendelea kuboresha mifumo ya usajili wa vyeti vya kuzaliwa, vifo, ndoa, talaka na vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi, na kuwasihi wananchi kufika ofisini kwa ajili ya kupata huduma hizo kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Kaskazini Unguja, Inspekta Salum Khamis Machano, akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa huo, aliwahimiza wazazi, walezi na walimu kushirikiana katika kupambana na utoro wa wanafunzi na kuhakikisha wanaripoti matukio yote ya udhalilishaji.
Alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwa karibu na watoto wao na kufuatilia mienendo yao ili kuwakinga dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji.



