Popular services

DKT. MZURI: WAANDISHI PAZENI SAUTI KUILINDA HESHIMA NA HAKI ZA WANAWAKE KUELEKEA UCHAGUZI 2025.


Na Nishan Khamis – Zanzibar

Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao kama silaha ya kutetea haki na heshima ya wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi kwa kuripoti na kukemea kwa nguvu zote vitendo vya udhalilishaji na vurugu, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa, katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika jana katika ofisi za chama hicho zilizopo Tunguu, yakiwahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari visiwani Zanzibar.

Dkt. Mzuri amesema kuwa waandishi wana nafasi ya kipekee ya kuhakikisha wanawake wanapata nafasi katika ulingo wa siasa bila kukumbana na aina yoyote ya manyanyaso au hofu.

Ameeleza kuwa licha ya kuwepo kwa sheria na sera nzuri kama Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2023 na Sera ya ZEC ya mwaka 2015 ambazo zinatoa msukumo kwa ushiriki wa wanawake, bado utekelezaji wake unahitaji kuimarishwa ili kuwalinda ipasavyo wanawake katika shughuli zao za kisiasa.

Aidha, amewataka waandishi kuchunguza na kuripoti kwa kina kuhusu changamoto ya rushwa, ambayo imekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake kufikia ndoto zao katika uongozi, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi. Pia amewahimiza kuandika habari na makala chanya za mafanikio ya wanawake katika nyanja mbalimbali ili kuwa motisha kwa wanawake wengine wanaotamani kuingia kwenye uongozi.

Kwa upande wake, Afisa Mawasiliano Khairat Haji kutoka TAMWA ZNZ alizungumzia udhalilishaji wa wanawake kupitia mitandao ya kijamii una athari kuwa kisaikolijia akieleza kuwa mazoea ya kutoa lugha za matusi na kejeli zinazolenga mwonekano au maisha binafsi ya mwanamke ni aina ya ukatili unaopaswa kulaaniwa na kukemewa vikali.

Hivyo ametoa wito kwa waandishi na jamii kwa ujumla kupinga vita vitendo vya udhalilishaji wa kimtandao ili kulinda heshima na haki za wanawake nchini kwa kuwawezesha wanawake kufikia ndoti zao za kisasa na uongozi.

Baadhi ya waandishi walioshiriki mafunzo hayo walitoa pongezi kwa TAMWA ZNZ kwa kuwawezesha kupitia mafunzo hayo, wakieleza kuwa yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu wajibu wao katika kulinda haki za wanawake. Waliahidi kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii juu ya haki ya mwanamke ya kuchagua na kuchaguliwa.

Mafunzo hayo yaliratibiwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), yakilenga kuhamasisha waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele katika kuripoti na kukemea vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.