Popular services

UWT NA DAS WATEKELEZA AHADI YA KUKABIDHI MAJIKO YA GESI KWA WANAWAKE WAJASIRIAMALI WADOGO KILINDI


Na: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja

Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kushirikiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, leo wametekeleza ahadi ya kukabidhi majiko ya gesi kwa wanawake wajasiriamali wadogo katika kijiji cha Kilindi, Jimbo la Nungwi.

Akikabidhi majiko hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja Mariam Said Khamisi, alisema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia sera yake ya matumizi ya nishati safi kwa Watanzania. Alisema ni sehemu ya kampeni ya marais wote nchini ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwawekea mazingira bora ya ujasiriamali mdogo.

Aidha, alieleza kuwa utekelezaji huo umetokana na ahadi iliyotolewa katika ziara ya Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, Bi. Zainab Shomar, na DAS, wakati wa kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura katika wilaya hiyo.

Bi. Zainab Shomar aliahidi kuwapatia wajasiriamali hao majiko ya gesi kama njia ya kuwaunga mkono katika matumizi ya nishati safi na kuwaepusha na madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kuni.

Kwa upande wake, DAS aliwahamasisha wanawake hao kuendelea kutumia majiko hayo ya gesi kwa uendelevu, huku akitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwapigia kura viongozi waliopo madarakani. Pia aliwataka kujitokeza kwa wingi katika mbio za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika tarehe 20 mwezi huu katika wilaya hiyo.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu wa Sheha wa Nungwi, Khamis Kibata kwa niaba ya Sheha wa Kilindi, alisema kuwa kutokana na ongezeko la wajasiriamali wanawake katika shehia hiyo, msaada huo wa majiko utasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda afya na kuongeza usalama wa mazingira ya kazi zao.

Akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali, Bi. Helta Eliaus Salum alitoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, UWT na DAS kwa msaada huo. Alisema amekuwa akisumbuliwa mara kwa mara na matatizo ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kuni, hivyo ujio wa majiko ya gesi utaboresha afya na ufanisi wa kazi zao.
Aidha, alitoa ombi kwa serikali na wadau kuendelea kuwasaidia wanawake wajasiriamali katika fursa mbalimbali ili waweze kujiimarisha zaidi kiuchumi. Alisisitiza kuwa wao kama wanawake wako tayari kujitokeza na kupiga kura za ndiyo kwa Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi mwezi Oktoba