Popular services

NAPAC YAJIKITA KUTOA ELIMU YA KISHERIA, KUSIKILIZA CHANGAMOTO ZA KISHERIA KWA WAKAAZI WA MKOKOTONI


Na: Nishan Khamis – Kaskazini Unguja

Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), imeendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wakazi wa Shehia ya Mkokotoni kupitia kliniki ya msaada wa sheria (Legal Aid Clinic), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa LEAP II (Legal Empowerment and Access to Justice Program) unaofadhiliwa na UNDP.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mkurugenzi wa NAPAC, Asia Fadhil Makame, alisema taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2016 na kusajiliwa rasmi mwaka 2017, inalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao za kisheria ili waweze kuzifikia kwa ajili ya maendeleo ya jamii.

“Tunaendelea kutoa huduma mbalimbali kama vile usuluhishi wa migogoro midogo, ushauri wa kisheria na elimu ya sheria kwa jamii bila gharama yoyote,” alisema Asia, akihimiza wananchi kushirikiana na NAPAC kutatua changamoto zinazowakabili kisheria.

Kwa upande wake, Afisa Mfuatiliaji na Tathmini wa NAPAC, Khamis Kombo Ali, alisema mradi huo unalenga kuwawezesha wananchi katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kisheria kwa msingi wa haki, amani na ushirikiano wa maendeleo ya taifa.

Katika mkutano huo, baadhi ya wananchi wa Mkokotoni walieleza changamoto kadhaa zinazowakabili, ikiwemoUwepo wa jengo bovu linalochochea vitendo vya uhalifu kama uuzaji wa dawa za kulevya, wizi na udhalilishaji,Changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa na vyeti vya kuzaliwa, ambayo imekuwa kikwazo katika kupata huduma muhimu.


Akijibu hoja hizo, Afisa wa Usajili wa Vizazi na Vifo Wilaya hiyo, Haji Ali Shamte, alisema ofisi yake inaendelea kuboresha mifumo ya usajili ili kutoa huduma kwa haraka na ufanisi zaidi. Aliwasihi wananchi kufika ofisini kwao kwa utatuzi wa changamoto hizo.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Kaskazini Unguja, Inspector Salum Khamis Machano, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Mkoa huo, aliwapongeza wananchi kwa kuibua changamoto zinazowakabili na kuahidi ushirikiano wa Jeshi la Polisi katika kuzitatua. Aliwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria hasa katika kesi za udhalilishaji ili kukomesha vitendo hivyo hatarishi.