Popular services

NAPAC YASAMBAZA ELIMU YA SHERIA NA KUSIKILIZA CHANGAMOTO ZA KISHERIA DONDE MUWANDA


Na: Nishan Khamis – Kaskazini Unguja

Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC), kwa kushirikiana na shirika la UNDP, imetoa msaada wa kisheria kwa wakazi wa Shehia ya Donge Muwanda kupitia kliniki ya msaada wa sheria (Legal Aid Clinic). Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa LEAP II (Legal Empowerment and Access to Justice Program) unaofadhiliwa na UNDP.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, Mkurugenzi wa NAPAC, Asia Fadhil Makame, alisema lengo kuu ni kuwaelimisha jamii kuhusu utambuzi wa haki na sheria katika nyanja mbalimbali, ili waweze kuzifikia haki zao za msingi kwa ajili ya maendeleo ya jamii.

Asia alieleza kuwa NAPAC inatoa huduma za msaada wa kisheria katika shehia zote 44 za Wilaya hiyo, zikiwemo huduma za usuluhishi wa migogoro midogo na ushauri wa kisheria, bila malipo. Aliihimiza jamii kushirikiana na taasisi hiyo kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili.

Naye Afisa Mfuatiliaji na Tathmini wa NAPAC, Khamis Kombo Ali, alieleza kuwa baada ya ufuatiliaji kijijini hapo, walibaini changamoto nyingi za kisheria. Kupitia ufadhili wa UNDP, wameamua kuongeza nguvu katika uwezeshaji wa jamii kwa elimu ya sheria ili wananchi waweze kufahamu haki zao za msingi, ikiwa ni pamoja na kutumia uhuru wa kujieleza kwa lengo la kuleta maendeleo.

Wananchi walieleza changamoto zinazowakabili kijijini hapo zikiwemo migogoro ya ardhi, magari ya mchanga yanayoharibu barabara, wizi na ulevi kwa vijana.

Haji Machano Makame maarufu kama Kamanda, alitaja tatizo la udhalilishaji kuwa bado ni changamoto kubwa. Alitoa wito kwa NAPAC na wadau wengine kufanya uchechemuzi wa sheria ili kuhakikisha zinatekelezwa kwa usawa, na kwamba wanaume wasiendelee kuwa waathirika kimyakimya, kwani baadhi ya matukio hutokana pia na wanawake.

Kwa upande wake, Inspector Salum Khamis Machano, Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Kaskazini Unguja, akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, aliahidi kufikisha changamoto za kiusalama kwa uongozi wa juu ili zichukuliwe hatua. Aliwahimiza wanaume kuripoti matukio ya udhalilishaji bila aibu, na jamii kwa ujumla kushiriki kutoa ushahidi kwenye kesi hizo ili kusaidia kutokomeza vitendo vya udhalilishaji.