Popular services

NAPAC YAWAFIKIA WAKAZI WA TUMBATU JONGOWE KWA KUTOA ELIMU NA MSAADA WA KISHERIA


Na: Nishan Khamis – Kaskazini Unguja

Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC), kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), leo imeendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wakazi wa kisiwa cha Tumbatu Jongowe kupitia kliniki ya msaada wa sheria (Legal Aid Clinic).

Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Afisa Tathmini wa NAPAC, Khamis Kombo Ali, amesema huduma hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa LEAP II (Legal Empowerment and Access to Justice Program) unaofadhiliwa na UNDP, ukiwa na lengo la kuwawezesha wananchi kupata haki zao kupitia elimu ya kisheria.

Akitoa mada katika mkutano huo, Salma Ibrahim kutoka NAPAC amesema suala la muhali limeendelea kuwa changamoto katika kisiwa hicho. Hivyo, ujio wa NAPAC unatoa fursa kwa jamii hiyo kuelewa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria, na kuhimiza jamii kuachana na muhali ili kutokomeza vitendo vinavyokwamisha maendeleo ya kijiji na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao, wananchi wa Tumbatu Jongowe wameishukuru NAPAC kwa msaada wa kisheria walioupata, wakiahidi kuchukua hatua dhidi ya tatizo la muhali. Pia, kuelekea kipindi cha uchaguzi, wamelitaka shirika hilo kuishauri mamlaka kusimamia ipasavyo vitendo vya udhalilishaji vinavyoongezeka wakati wa kampeni, pamoja na kushughulikia changamoto ya vyeti vya kuzaliwa kwa watoto, jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa familia nyingi.

Akijibu maswali ya wananchi, Mkurugenzi wa NAPAC, Bi. Asia Fadhil Makame, amewashauri wazazi kuwa karibu na watoto na vijana wao hususan wakati wa uchaguzi, kwani kipindi hicho huchangia kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji kutokana na baadhi ya wazazi kutojikita kikamilifu katika malezi. Pia ameahidi kuwa taasisi yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutatua changamoto ya vyeti vya kuzaliwa.