Popular services

NAIBU KATIBU MKUU WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM AWASISITIZA WANANCHI KUTUNZA AMANI NA KUJITOKEZA KWA WINGI SIKU YA KUPIGA KURA


Na, Nishan Khamis – Wilaya ya Kaskazini A, Unguja | Alhamisi, 21 Agosti 2025

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania -Zanzibar, Ali Issa Ali, amewataka wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kutunza amani, kudumisha utulivu na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura kwa kufuata kanuni na sheria za uchaguzi, kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar kwa ujumla.

Naibu Ali aliyasema hayo katika ziara yake wilayani Kaskazini A, Unguja alipokutana na wavuvi, wakulima na waendeshaji boda boda kutoka shehia za Matemwe Kigomani na Mkwajuni. Alisema lengo kuu la ziara hiyo ni kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na kuwachagua viongozi wa CCM ili chama hicho kiendelee kushika dola na kuleta maendeleo zaidi nchini.

Amesema CCM ni chama cha amani na maendeleo, hivyo wananchi wana kila sababu ya kuendelea kukichagua ili kuimarisha ustawi wa taifa. Alisisitiza pia umuhimu wa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa amani na utulivu.

Aidha, aliwahakikishia wananchi kwamba Ilani ya CCM 2025–2030 imeweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha kiuchumi makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo wavuvi, wakulima na waendesha boda boda, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Kaskazini A, Jafar Mohammed Khamis, alisema anashukuru kwa wilaya hiyo kuendelea kudumisha amani na mshikikano, na kuongeza kuwa ujio wa ziara hiyo ni chachu ya kuimarisha mshikikano wa chama na kuongeza uungwaji mkono kwa juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Nao baadhi ya wanachama wa CCM walisema wataendelea kuwa mabalozi wa amani na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, ili kuhakikisha chama hicho kinaendeleza dola na kuimarisha maendeleo nchini.