Popular services

NAPAC YAWANOA MTAKUWWA DHIDI YA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WILAYA YA KASKAZINI 'A' UNGUJA.


Nishan Khamis – Gamba
Jumapili, 10 Agosti 2025

Kamati ya Kupambana na Vitendo vya Udhalilishaji Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, imewahimiza maafisa na jamii kuendeleza ushirikiano na Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria (NAPAC) ili kutokomeza vitendo hivyo katika jamii.

Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha maafisa wa wilaya na wanaharakati wa kupinga udhalilishaji, Maafisa Ufuatiliaji na Tathmini wa NAPAC, Khamis Kombo Ali na Hadia Ali Makame, walisema kuwa licha ya kuongezeka kwa elimu na mwamko wa kuripoti matukio, bado vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake, watu wenye ulemavu na watoto vinaendelea kushuhudiwa. Wameeleza kuwa hali hiyo inahitaji mshikamano wa pamoja ili kutokomeza vitendo hivyo vyenye athari kubwa kwa wahanga, jamii na taifa kwa ujumla.

Walisema kamati hiyo imeundwa kupitia mradi wa Sauti ya Mwanamke katika Utalii, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia ENABEL na LSF, na kwamba mradi huo utasaidia kwa kiwango kikubwa mapambano dhidi ya udhalilishaji.

Kwa upande wao, wajumbe wa kikao walibainisha kuwa licha ya juhudi kubwa za kutoa elimu na kufuatilia kesi, bado kuna changamoto za muhali miongoni mwa wahanga na ukosefu wa ushirikiano mzuri kutoka kwa baadhi ya mamlaka zinazoshughulikia kesi hizo, jambo linalokwamisha mapambano.

Aidha, Afisa wa Watu Wenye Ulemavu wa wilaya hiyo, Khamis Rashid Khamis, alisema kuwa hadi sasa hajapokea kesi za udhalilishaji zinazohusisha kundi hilo. Hata hivyo, alibainisha kuwa hali hiyo haimaanishi kuwa vitendo hivyo havifanyiki, bali ni ishara kwamba baadhi ya wahanga bado wana muhali wa kuripoti. Alisisitiza umuhimu wa jamii kujitokeza kuripoti matukio hayo ili kuhakikisha upatikanaji wa haki na usawa kwa watu wenye ulemavu.

Akifunga kikao hicho, Mkurugenzi wa NAPAC Wilaya ya Kaskazini A, Asia Fadhil Makame, alisema lengo la mkutano huo ni kujengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia (MTAKUWWA) ya wilaya hiyo. Alisema walengwa wa mradi ni makundi maalum, ikiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu, na kusisitiza haja ya kuandaa mikakati madhubuti ya pamoja ili kuwalinda na kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu madhara ya vitendo vya udhalilishaji.