Popular services

RC MATTAR: RAIS MWINYI AMEIBADILISHA KASKAZINI,AELEZA MIKAKATI YA KIMAENDELEO YA MKOA.


Na Nishan Kamis, Kaskazini Unguja .
 Jumatatu, 18 Agosti 2025

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, amesema wananchi wa mkoa huo wana kila sababu ya kumpongeza na kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kasi kubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali.

Akizungumza ofisini kwake Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Mkono wa Mshua, Mhe. Mattar alisema kampeni hiyo inalenga kuonesha mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi.

Amesema katika sekta ya maji, tangu Rais Mwinyi aingie madarakani, upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka lita milioni 15 hadi kufikia zaidi ya lita milioni 21, sawa na asilimia 70 ya mahitaji ya mkoa huo. Hata hivyo, amekiri bado changamoto ipo katika maeneo ya Nungwi, Kendwa, Pwani Mchangani na maeneo mengine, ambapo Serikali tayari imechukua mkopo wa dola milioni 26 kutoka Serikali ya Oman kwa ajili ya kuchimba visima na kulaza mabomba mapya.

Aidha, katika sekta ya elimu, Mhe. Mattar alisema Rais Mwinyi amejenga madarasa 670, shule za ghorofa, mabweni na ofisi za maafisa elimu, na pia amedhamiria kujenga shule nyingine sita za ghorofa pamoja na nyumba za walimu ili kuimarisha zaidi elimu katika mkoa huo.

Kwa upande wa miundombinu, amesema barabara zenye urefu wa kilomita 117.73 tayari zimejengwa, huku ujenzi wa kilomita 41.54 ukiendelea. Akimaliza mwaka huu, jumla ya barabara zitakazokamilika zitafikia kilomita 160, kiwango kinachokaribia malengo ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025.

Aidha, amesema Serikali imewezesha wanawake na vijana kwa kuwapatia mitaji na elimu ya kifedha, jambo lililoongeza uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Pia vijana wamepata nafasi ya kushiriki katika programu za ajira kupitia miradi ya ujasiriamali na miundombinu.

“Kwa mafanikio haya na mengineyo, nimezindua kampeni ya Mkono wa Mshua kama ishara ya kuenzi kasi ya maendeleo na uongozi wa busara wa Rais Dk. Mwinyi. Kampeni hii ni alama ya mshikamano na dira ya maendeleo ya Zanzibar,” alisema Mhe. Mattar.

Kwa upande wao, waandishi wa habari walimpongeza Rais Mwinyi kwa maendeleo yanayoonekana mkoani humo na kuahidi kushirikiana na uongozi wa mkoa katika kuhabarisha umma kuhusu mafanikio hayo.