Na, Nishan Khamis – Mkwajuni
Alhamisi, 14 Agosti 2025
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, imelaani vikali kitendo cha baadhi ya viongozi watia nia wa nyadhifa za uongozi kuendelea kusambaza taarifa za uzushi zinazotia doa chama na jimbo, mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kura za maoni ndani ya chama hicho.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Siasa na baadhi ya watia nia wa uongozi katika jimbo hilo uko mkwajuni jimboni, Katibu wa CCM Jimbo la Mkwajuni, Juma Mshenga Juma, amesema taarifa za upotoshaji zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii na katika maskani mbalimbali ni kinyume na taratibu za chama.
Ameeleza kuwa vitendo hivyo, pamoja na kuundwa kwa makundi yasiyo na tija, ni ukiukaji wa Katiba ya chama, na ametoa wito kwa wanachama wote wa CCM kupuuza taarifa hizo za uongo na kushirikiana kwa umoja ili chama kiendelee kushinda kwa kishindo na kuendelea kushika dola nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa jimbo hilo, Khamis Makame Khamis, amesema kuwa yeyote atakayekwenda kinyume na Katiba ya chama atachukuliwa hatua stahiki kulingana na kanuni na sheria za CCM.
Amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano ndani ya chama ili kuhakikisha Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wake Dk. Hussein Ali Mwinyi, na viongozi wengine wa chama wanashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.
Baadhi ya watia nia na wajumbe wa Kamati ya Siasa waliopata nafasi ya kuzungumza wamepongeza hatua ya kuitisha kikao hicho na kulaani vitendo vya uzushi vinavyofanywa na baadhi ya watia nia, huku wakiitaka Kamati ya Siasa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika na hatia.
