Alhamisi, 7 Agosti 2025
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A Unguja, leo imefanya kikao na kutoa tamko la kufuatilia kwa umakini uwepo wa baadhi ya makundi ndani ya chama hicho yanayodaiwa kuleta mtafaruku katika mchakato wa uteuzi wa mgombea wa ubunge wa jimbo hilo, mara baada ya kuteuliwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza na watia nia wa nafasi mbalimbali katika jimbo hilo, Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Nungwi, Bw. Ali Habibu Mtwana, ameshukuru kwa kumalizika kwa amani na utulivu katika zoezi la kura za maoni, ambalo amesema lilifanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia kanuni zote za uchaguzi wa chama.
Hata hivyo, amebainisha kuwa mara baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, zimeanza kuonekana taarifa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikionesha dalili za uvunjifu wa amani na mshikamano wa chama, pamoja na kuibuka kwa makundi yenye malengo yasiyo na tija kwa ustawi wa chama hicho katika jimbo hilo.
Amesema CCM ina katiba na kanuni madhubuti zinazoongoza uteuzi wa viongozi, na kwamba kila mwanachama ana wajibu wa kumuunga mkono na kushirikiana na mgombea atakayeteuliwa rasmi na Kamati ya Siasa ya Mkoa, ili kwa pamoja kutekeleza ilani ya CCM na kuendeleza maendeleo ya chama na taifa kwa ujumla.
Bw. Mtwana ameongeza kuwa kamati hiyo inaendelea na uchunguzi wa kina, na endapo watabaini wahusika wa kuanzisha au kuchochea makundi yenye kuathiri mshikamano wa chama, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa.
Ametoa wito kwa wanachama wa CCM Jimbo la Nungwi kuendelea kushirikiana na kuepuka siasa za makundi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola.
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa jimbo hilo, Bw. Habibu Ali Shaha, amesisitiza kuwa CCM ina taratibu na kanuni za ndani ambazo kila mwanachama anatakiwa kuziheshimu. Amesema masuala yote yanapaswa kushughulikiwa kwa kufuata utaratibu wa kisheria wa chama badala ya kuanzisha makundi yatakayopelekea kuonekana kwa taswira hasi ya chama hicho katika jimbo hilo.
Wajumbe wa kikao hicho wametoa pongezi kwa uongozi wa jimbo kwa hatua zilizochukuliwa, na wameahidi kuendelea kushirikiana ili chama kiendelee kuwa imara kwa maendeleo ya jimbo, mkoa na taifa.
Kikao hicho kimehusisha Kamati ya Siasa ya Jimbo la Nungwi, wajumbe, na watia nia wote wa nafasi za udiwani, uwakilishi na ubunge, ambapo masuala ya mshikamano na umoja wa chama yalijadiliwa kwa kina huku ikisisitizwa kuachana na siasa za makundi.
