Alhamisi, 7 Agosti 2025
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, amewasihi vijana wa mkoa huo kuchagua viongozi bora katika uchaguzi mkuu ujao na kujiepusha na viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani kabla na baada ya uchaguzi.
Mhe. Mattar alitoa wito huo leo katika viwanja vya Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, wakati wa kongamano la shamrashamra za maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani lililoandaliwa na shirika la ActionAid kwa kushirikiana na Taasisi ya Juvieka.
Amesema vijana wana nafasi kubwa ya kudumisha amani na kulinda taifa, hivyo wanapaswa kuepuka vitendo vyote vya vurugu na badala yake kuwa mabalozi wa amani kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pale wanapobaini viashiria vya uvunjifu wa amani.
Aidha, Mhe. Mattar ameipongeza Juvieka kwa jitihada zao zenye maslahi ya maendeleo ya vijana, akibainisha changamoto ya upungufu wa nafasi za ajira katika sekta ya mahoteli mkoani humo. Ameeleza kuwa ofisi yake imeandaa mikakati madhubuti ya kushughulikia changamoto hiyo ili vijana wanufaike na fursa zilizopo, huku akisisitiza kuwa ajira kwenye sekta ya utalii si kikwazo cha kuvunja mila na silka za Mzanzibari.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Bw. Ali Haji Hassan, amewataka vijana kushiriki ipasavyo kwenye uchaguzi na kulinda amani. Pia amewahimiza kubadili mtazamo na kukimbilia fursa za maendeleo kwa kujiunga na mabaraza ya vijana na taasisi mbalimbali ili kuwa na sauti moja yenye ushawishi.
Naye Mkurugenzi wa Juvieka, Bw. Mbarouk Maalum Mohammed, amesema kongamano hilo limehudhuriwa na vijana 116 kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na wawakilishi wa mabaraza ya vijana, taasisi na wadau mbalimbali. Mada mbili zimewasilishwa—Ushiriki wa Vijana kwenye Uchaguzi na Kudumisha Amani na Changamoto za Wanawake na Vijana kwenye Sekta ya Utalii. Kaulimbiu ya mwaka huu kwa upande wa Zanzibar ni: “Vijana Tunaweza – Tutashiriki Kuchagua na Kuchaguliwa.”
Bw. Mbarouk ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa, shirika la ActionAid, mabaraza ya vijana, na taasisi zilizoshiriki katika kujadili changamoto na kutafuta suluhu kwa maendeleo ya vijana, mkoa na taifa kwa ujumla.
Washiriki wa kongamano hilo wamepongeza Juvieka kwa kutoa jukwaa la kujadili masuala muhimu ya vijana. Wamesema mila na silka za Mzanzibari mara nyingi zinatajwa kama kikwazo kwa vijana na wanawake kukimbilia fursa za ajira katika mahoteli, jambo linalokwamisha maendeleo yao. Wameitaka jamii kubadili mtazamo huo, kwani sekta ya hoteli pia ina nafasi za ajira zenye heshima na zinazozingatia maadili ya Kizanzibari.

