Popular services

RC MATTAR AKABIDHI VYAKULA VYA KAMBI KWA WANAFUNZI, AHIMIZA USHIRIKIANO KUKUZA UFAULU


Na,Nishan khamis- kaskazini Unguja

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mheshimiwa Mattar Zahor Masoud, amekabidhi msaada wa vyakula kwa wanafunzi wa kambi za kitaaluma katika Mkoa wake na kuhimiza mshikamano wa pamoja kati ya wazazi, walimu na jamii kwa ujumla ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo   skuli ya mkokotoniwilayayakaskaziniAUnguja, RC Mattar alisema msaada huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ikiwa ni mwendelezo wa programu ya Mkono wa Mshua yenye lengo la kusimamia kwa vitendo maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Alifafanua kuwa vyakula vilivyotolewa ni pamoja na mchele, maharage, mafuta ya kupikia, sukari na unga, ambavyo vitasaidia kuimarisha huduma za chakula katika kambi za kitaaluma na kuwajengea wanafunzi mazingira mazuri ya kujisomea.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa mshirikiano wa karibu baina ya wazazi, walimu na walezi katika malezi ya kitaaluma, akibainisha kuwa mshikamano wa pamoja ndio nguzo ya kupata matokeo bora ya kitaaluma.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mussa Said Salum, aliishukuru Serikali kwa msaada huo na kueleza kuwa utakuwa nyenzo muhimu katika kuongeza morali ya wanafunzi na hatimaye kuinua kiwango cha ufaulu.

Nao wajumbe wa kamati za skuli walisema msaada huo ni kielelezo cha dhamira njema ya Serikali katika kuhakikisha elimu inapata nafasi ya kipekee, na wakaahidi kuusimamia kikamilifu ili uwanufaishe wanafunzi waliokusudiwa.