Na, Nishan Khamis – Kaskazini Unguja
Jumanne, 19 Agosti 2025
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, inaendelea kuimarisha sekta ya michezo kwa kujenga viwanja vya michezo katika wilaya zote za mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, RC Mattar alisema ujenzi wa viwanja hivyo umefikia asilimia 80, ambapo kiwanja kimoja kinajengwa Kitope, Wilaya ya Kaskazini B, na chengine kipo Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A.
Amesema michezo ni moja ya sekta zinazotoa ajira ndani na nje ya nchi, hivyo kukamilika kwa viwanja hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuibua vipaji vya vijana na kutengeneza fursa mbalimbali kupitia michezo.
Aidha, RC Mattar alibainisha kuwa suala la ushiriki wa watu wenye ulemavu lizingatiwa katika ujenzi wa viwanja hivyo, jambo litakalowapa nafasi ya kuonesha uwezo, vipaji na ujuzi wao katika sekta ya michezo.
Vilevile ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kumuunga mkono Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi ili aendelee kuimarisha maendeleo ya mkoa huo.
Kwa upande wao, wadau wa michezo walisema wamefarijika na hatua ya ujenzi wa viwanja hivyo, wakieleza kuwa ni ishara njema ya dhamira ya Rais Dk. Mwinyi kuboresha miundombinu ya michezo. Wameahidi kuendelea kumpa ushirikiano ili sekta hiyo iweze kukua kwa manufaa ya mkoa na Zanzibar kwa ujumla.
