Popular services

Madaktari na Wanafunzi wa Afya SUZA Wafanikisha Uchunguzi wa Kisukar na Shinikizo la Damu Matemwe Kaskazini


Matemwe Kaskazini, Zanzibar – Nishan Khamis, 31 Agosti 2025

Madaktari na wanafunzi wa afya kutoka Chuo cha Bweni SUZA wamefanya programu ya uchunguzi wa maradhi ya kisukar na shinikizo la damu kwa wananchi wa kijiji cha Matemwe Kaskazini, wakiwafikia watu 160 na kuwapa matibabu pamoja na elimu ya afya.

Daktari Gora Faki Haji, Mhadhiri wa Chuo hicho, ambaye pia ni mbobezi wa Afya ya Jamii (Public Health Specialist), alisema kuwa lengo la programu hii ni kufikia watu 200. “Uchunguzi wa mapema ni njia bora ya kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na maradhi haya. Tunawaomba wananchi kuwa na utaratibu wa kuchunguza afya zao mara kwa mara,” alisema Dkt. Gora.

Dokta Gora amesema serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt Husein Ali Mwinyi imeimarisha miundombinu ya afya kila sehemu nchini ivyo programu hiyo ni kuunga mkono juhudi za rais katika kutatua changamoto za kiafya kwa wanajamii nchini.

Mwanafunzi wa Udaktari wa chuo ch Afya Mbweni SUZA Sharahabil Hamad na Samha Suleiman Yusuf, walitoa Elimu ya Afya ya Shinikizo la Damu na Kisukari. Waliwatajia wananchi hao vichocheo (risk factors) ikiwemo, uzito uliopitiliza, mirathi(yaani genetics or family history), umri, upungufu wa mazoezi na ulaji wa vyakula bila mpangilio maalum kama vile chumvi nying na mafuta vinaweza kuchangia kupata magonjwa hayo.

Wanafunzi hao pia walisisitiza hatua za kuchukua pale dalili hizi zinapotokea, ikiwa ni pamoja na kuchunguza afya mara kwa mara, kubadilisha lishe na kula vyakula vyenye sukari kidogo na chumvi kidogo, kufanya mazoezi ya mwili kwa utaratibu, kuepuka matumizi ya pombe na sigara, na kufuata ushauri wa madaktari. Walisisitiza kuwa utambuzi wa mapema unasaidia kupunguza madhara makubwa na kuzuia matatizo ya moyo na figo.

Mkurugenzi wa Kauthar Specialized Clinic na mfadhili wa programu hiyo, Juma Machano, alisema kuwa jamii za vijiji zinakumbana na changamoto mbalimbali za kiafya. “Programu hii imegusa jamii moja kwa moja na kuona sehemu sahihi ya kuendeleza juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Dkt. Husein Ali Mwinyi katika sekta ya afya nchini,” aliongeza.

Katibu wa sheha Shehia ya Matemwe Kaskazini kidawa Khatib Haji alishukuru kwa uchaguzi wa kijiji chao kuwa sehemu ya programu hii yenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha elimu ya afya kwa wakaazi. Aidha, aliwatoa wito wananchi kuendelea kushiriki katika mpango wa uchunguzi wa afya na kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazowakabili zinatatuliwa kwa ushirikiano wa pande zote.

Programu hii imeonekana kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, ikiwasaidia wananchi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu maradhi ya kisukar na shinikizo la damu na njia za kujikinga.