Jumamosi 23-08-2025.
Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A Unguja (NAPAC) imewasilisha ripoti ya robo mwaka ya utekelezaji wa shughuli zake ikionesha kwamba jumla ya watu 5,279 wamefikiwa kupitia msaada na elimu ya kisheria pamoja na utatuzi wa changamoto zinazohusiana na udhalilishaji.
Akizungumza katika hafla ya uwasilishaji wa ripoti hiyo katika ukumbi wa mikutanoTCMkwajuni, Mkurugenzi wa NAPAC Wilaya hiyo, Asia Fadhil Makame, alisema taasisi yake imeendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji nchini.
Kwa upande wake, Mgeni rasmi Afisa Elimu wa Wilaya hiyo, Juma Mwadin Abdalla, aliipongeza NAPAC kwa jitihada za kusaidia jamii hususan wanawake, watoto na watu wenye ulemavu. Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kutokomeza vitendo vya udhalilishaji na kupaza sauti za makundi yaliyo hatarini.
Afisa Tathmini wa NAPAC, Hadia Ali Makame, akiwasilisha ripoti hiyo, alisema kati ya watu waliopatiwa msaada na elimu ya kisheria, wanawake walikuwa 2,794, wanaume 1,995 na watoto 490.
Aidha, Afisa wa Watu Wenye Ulemavu Wilaya hiyo, Khamis Rashid Khamis, alieleza kuridhishwa kwake na namna ripoti hiyo ilivyowajumuisha watu wenye ulemavu, akisisitiza haja ya jamii kuendelea kuwashirikisha katika nyanja zote.
Uzinduzi wa ripoti hiyo ulihudhuriwa na maafisa kutoka serikalini, asasi za kiraia, masheha na wadau wa masuala ya udhalilishaji. Tukio hilo limefanyika chini ya Mradi wa Sauti ya Mwanamke katika Utalii, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia ENABEL na LSF.

