Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imetoa msamaha wa asilimia 100 kwa madeni ya adhabu na riba kwa walipakodi watakaokidhi vigezo kwa utaratibu maalumu.
Akizungumza katika mafunzo maalum ya mabadiliko ya sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi, Makame Khamis Moh’d, alisema lengo la msamaha huo ni kusafisha mifumo na kuweka sawa taarifa za walipakodi, sambamba na kuwapa nafasi ya kuwajibika kwa hiari na kwa wakati.
Akitaja maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko hayo ya sheria za kodi, Makame alisema ni pamoja na kuimarisha uzalishaji wa viwanda vya ndani, udhibiti wa forodha, usimamizi wa vyombo vya moto, huduma jumuishi za kifedha, na ukusanyaji wa mapato yenye kodi na yasiyo na kodi.
Alifafanua kuwa mabadiliko hayo yametokana na haja ya kuwa na sheria zinazokwenda na wakati, mwenendo wa biashara, mabadiliko ya kiteknolojia, changamoto za utekelezaji, na malengo ya serikali.
Sheria zilizofanyiwa marekebisho kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ni pamoja na Sheria ya Mamlaka ya Mapato Zanzibar ya mwaka 2022, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Na. 8 ya mwaka 2017, na Sheria ya Fedha Na. 9 ya mwaka 2015.
ZRA imetoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya Zanzibar pamoja na kuwaomba wanahabari kuendelea kueneza habari izo kwa wananchi kwa maendeleo ziada ya Zanzibar.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya waanachi na wafanya biashara mkoa wa kaskazini Unguja wemepotoa pongezi za dhati kwa serikali na mamlaka kwa ujumla kwa msamaha huo huku walisisitiza kuwa wataendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya Zanzibar.

