Popular services

 Mwandishi:Nishan Khamis,Zanzibar.

Kijini, Matemwe.
Naibu Meya wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Kijiji katika Jimbo la Kijini, Faki Zuber Haji(Bera), amefanya ziara ya kikazi katika Kijiji cha Kijini Matemwe kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Katika ziara hiyo, Naibu Meya amekabidhi mipira ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho ili kusaidia kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama ambayo ilikuwa ni changamoto kwa muda mrefu.

Aidha, ametoa msaada wa bati kwa mwananchi aliyepatwa na maafa baada ya nyumba yake kuezuliwa na upepo mkali, hatua iliyolenga kumsaidia kurejesha makazi yake na kupunguza athari za maafa hayo.

Vilevile, amekabidhi ukindu kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali wa Kijini Matemwe ikiwa ni sehemu ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali.

Ameleza kuwa serikali itaendelea kusimamia na kuimarisha huduma za kijamii pamoja na kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto zao ili kuleta maendeleo endelevu katika maeneo yao. Alisisitiza kuwa uongozi wa karibu na wananchi ni msingi muhimu wa maendeleo.

Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Kijini Matemwe, Msiakwe Makame Haji, alieleza kufurahishwa na ziara hiyo na kupongeza juhudi za Naibu Meya kwa kuendelea kuwajali wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa wakati.

Aidha, wanakijiji wa Kijini Matemwe wameeleza kuridhishwa na msaada huo, wakisema umewasaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili hususan katika huduma ya maji, makazi na uwezeshaji wa vikundi vya wanawake.
Ziara hiyo iliambatana na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi tofauti katika Jimbo la Kijini, ambao walishiriki katika shughuli hiyo ya kuwatembelea wananchi na kusikiliza changamoto zao.