Mwandishi: Nishan Khamis, Zanzibar
Timu ya Nungwi City imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Wilaya ya Kaskazini A msimu wa mwaka 2025/2026 baada ya kukusanya alama 24 katika michezo 10 iliyocheza. Timu hiyo ilionyesha kiwango bora katika hatua ya nne bora kwa kushinda michezo mitatu na kuibuka kinara kati ya jumla ya timu 11 zilizoshiriki ligi hiyo.Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa mabingwa hao, Mkurugenzi wa NAPAC Asia, Fadhil Makame, aliipongeza Nungwi City kwa mafanikio hayo makubwa na kueleza kuwa michezo ni nyenzo muhimu katika kukuza vipaji, kuimarisha afya za vijana na kuleta mshikamano katika jamii.
Alisema kuwa serikali ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imeendelea kuweka mazingira bora ya kuendeleza sekta ya michezo nchini kwa lengo la kuinua vipaji vya vijana na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kaskazini A (NOAFA), Bakar Musa Vuai, alisema ligi hiyo imekuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana wengi na kuongeza ushindani wa soka katika wilaya hiyo. Alizipongeza timu zote zilizoshiriki kwa kuonesha nidhamu na ushindani wa hali ya juu katika msimu mzima wa ligi.
Kocha Mkuu wa Nungwi City, Simai Sheha Haji, alisema siri ya mafanikio ya timu hiyo ni nidhamu, kujituma kwa wachezaji, mshikamano pamoja na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi. Aidha,ametoa shukrani za dhati kwa wadhamini wa timu hiyo, Sister Island, kwa mchango wao mkubwa ulioiwezesha timu kufikia mafanikio hayo.
Katika hafla hiyo, mabingwa Nungwi City walikabidhiwa kombe, jozi mbili za jezi pamoja na mipira miwili. Mshindi wa pili, Kibuyuni FC, alipatiwa jezi na mipira miwili. Timu hizo ziliomba kuongezewa msaada wa vifaa vya michezo ili kusaidia maendeleo ya soka na kuinua vipaji vya vijana katika wilaya hiyo.