Mwandishi:Nishan Khamis, Zanzibar
Shirika la ActionAid Zanzibar limesema kuwa utekelezaji wa programu ya maji safi na salama mashuleni ni moja ya mikakati muhimu inayolenga kupunguza na kuondoa vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanafunzi katika mikoa ya Kaskazini Unguja na Kusini Unguja.Kauli hiyo ilitolewa na Mratibu wa ActionAid Zanzibar, Bakar Khamis Bakar, wakati wa bonanza la mashindano ya sanaa na mdahalo kwa wanafunzi wa shule za msingi lililofanyika katika Skuli ya Msingi Fujoni, Wilaya ya Kaskazini B.
Bakar amesema kuwa upatikanaji wa maji safi, salama na huduma bora za vyoo mashuleni huchangia kwa kiasi kikubwa kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia na kuimarisha usalama wa wanafunzi, hususan wasichana.
Ameeleza kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya elimu ili kuhakikisha vitendo vya udhalilishaji vinatokomezwa na haki za watoto zinalindwa.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mussa Said Salum, amelipongeza shirika la ActionAid Zanzibar kwa juhudi zake za kuunga mkono maendeleo ya elimu na kushiriki kikamilifu katika kampeni za kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa watoto.
Amesema Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imeendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu, jambo ambalo linapaswa kuambatana na juhudi za pamoja za kuhakikisha watoto wanalindwa, wanatunzwa na wanapata mazingira salama ya kujifunzia na kukuza vipaji vyao.
wanafunzi walioshiriki mashindano hayo wameeleza kufurahishwa na fursa waliyoipata kupitia bonanza hilo, wakisema limewasaidia kuonesha vipaji vyao, kuimarisha uwezo wa ubunifu na kutoa maoni yao kuhusu changamoto zinazowakabili watoto shuleni na katika jamii na mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwajengea ujasiri wa kuzungumzia masuala ya udhalilishaji na kutetea haki zao kwa njia ya sanaa na mdahalo.
Katika fainali za mashindano hayo, Skuli ya Bandamaji iliibuka mshindi wa nafasi ya kwanza katika kipengele cha mdahalo, huku Skuli ya Msingi Fujoni ikishika nafasi ya kwanza katika kipengele cha sanaa za maonyesho. Mashindano hayo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, yanayolenga kuhamasisha ulinzi, ustawi na maendeleo ya watoto barani Afrika.