Mwandishi, Nishan khamis, Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo, Mheshimiwa Cassian Gallos Nyimbo, amewataka walinzi shirikishi Jimbo la Chaani kuendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti viashiria vya uhalifu na kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu katika jamii.RC Gallos ameyasema hayo leo alipohudhuria mafunzo ya walinzi shirikishi wa Jimbo la Chaani yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shehia ya Mkorea, Jimbo la Chaani.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama mkoani humo pamoja na kuwajengea uwezo walinzi shirikishi katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mkuu wa Mkoa amesema walinzi shirikishi wana nafasi kubwa katika kusaidia juhudi za kuhakikisha usalama wa wananchi, kwa kuwa ni sehemu muhimu ya jamii inayoweza kubaini mapema viashiria vya uhalifu na kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Aidha, RC Gallos ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana katika kudhibiti viashiria na vitendo vyote vya udhalilishaji dhidi ya watoto na jamii kwa ujumla, hususan katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika.
Naye Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Ali, ametoa pongezi kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na wananchi kupitia walinzi shirikishi.
Amesema ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kuimarisha ulinzi na usalama Jimbo la Chaani na Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ujumla, huku akiahidi kuwa viongozi wataendelea kushirikiana na vyombo husika kwa maslahi mapana ya taifa.
Kwa upande wao, walinzi shirikishi wameshukuru kwa kupatiwa mafunzo hayo wakieleza kuwa yamewaongezea maarifa na uelewa wa kukabiliana na changamoto za kiusalama katika maeneo yao.
Wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uaminifu na uzalendo mkubwa ili kuendelea kusaidia juhudi za kulinda amani na usalama nchini.