Mwandishi. Nishan khamis. Zanzibar.
Wakulima wa mashamba ya Mto Maji Fungurefu yaliyopo Wilaya ya Kaskazini A wameiomba Serikali kutoa ufafanuzi kuhusu suala la fidia kufuatia mpango wa kuwaondoa katika maeneo hayo, wakisema bado hawajapata maelezo ya kutosha kuhusu hatima ya mashamba ambayo yamekuwa yakiwapatia riziki kwa muda mrefu.
Wakulima hao wamezungumza leo katika eneo la mashamba hayo baada ya kikao kilichowakutanisha na viongozi Wizara ya Uchumi wa Buluu, ambapo walieleza kutoridhishwa na baadhi ya maelezo yaliyotolewa kuhusu mustakabali wa maeneo hayo.
Pamoja na hilo, wameeleza wasiwasi wao juu ya shughuli za uchimbaji mchanga zinazoendelea katika eneo hilo, wakidai kuwa zimekuwa zikisababisha uharibifu wa mazao na kuathiri shughuli zao za uzalishaji wa kilimo.
Wamesema mashamba ya Mto Maji Fungurefu yana umuhimu mkubwa kwa wananchi wengi wa eneo hilo kwani ndiyo chanzo kikuu cha chakula na mapato kwa familia nyingi zinazoyategemea kwa maisha yao ya kila siku.
Aidha, wameiomba Serikali kuzingatia hali ya maisha ya wananchi wanaotegemea mashamba hayo kabla ya kuchukua maamuzi yoyote, wakieleza kuwa wengi wao hawana maeneo mengine ya kilimo wala vyanzo mbadala vya mapato.
Wamesisitiza umuhimu wa mazungumzo na ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato huo, wakiamini kuwa hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa suluhisho la haki na lenye kuzingatia ustawi wa wakulima pamoja na maendeleo ya eneo husika