Popular services

DKT. FARID MOHAMMED HAJI AAPISHWA KUWA KATIBU TAWALA WILAYA YA KASKAZINI A.

 

Na Nishan Khamis, Zanzibar
Katibu Tawala mpya wa Wilaya ya Kaskazini A, Dkt.Farid Mohammed Haji, leo ameapishwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Cassian Gallos Nyimbo, katika hafla iliyofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa viongozi, watendaji wa serikali na wananchi ili kumwezesha Katibu Tawala huyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Amesema ushirikiano huo utasaidia kuifanya Wilaya ya Kaskazini A pamoja na Mkoa wa Kaskazini Unguja kuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

Mhe. Cassian Gallos Nyimbo ameeleza kuwa maendeleo endelevu yanapatikana kupitia mshikamano, uwajibikaji na ushirikiano wa pamoja, huku akiwataka watendaji wa serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wake, Dkt. Farid Mohammed Haji ameshukuru kwa maandalizi mazuri ya hafla hiyo ya kuapishwa kwake, huku akitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, kwa imani aliyomuonesha kwa kumteua kushika nafasi hiyo.

Dkt. Farid ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na kujituma, na kusema kuwa atafanya kazi kwa karibu na viongozi, watendaji na wananchi ili kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Kaskazini A na Zanzibar kwa ujumla.

Aidha, ameomba ushirikiano kutoka kwa watendaji wenzake na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa manufaa ya wananchi.

Hafla ya kuapishwa kwake imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, watendaji wa umma na wadau wa maendeleo ofisi ya wilaya katika ,madiwani na wadau mbalimbali.