Popular services

 Mwandishi: Nishan Khamis, Zanzibar.

Jamii ya Shehia ya Mto wa Pwani, Wilaya ya Kaskazini A, imetakiwa kuimarisha ushirikiano katika kudhibiti wimbi la utoro wa wanafunzi pamoja na mporomoko wa maadili kwa watoto na vijana katika shehia hiyo.

Akizungumza na wananchi wa Shehia ya Mto wa Pwani, Mkurugenzi wa Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC), Asia Fadhil Makame, amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu mwenendo wa baadhi ya watoto na vijana, hali ambayo inahitaji ushirikiano wa pamoja ili kupata suluhisho.
Amesema malezi bora, ufuatiliaji wa karibu na ushirikiano kati ya wazazi, walimu, viongozi na jamii ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama yenye maadili mema.

Aidha, Asia ameeleza kuwa uwepo wa shughuli mbalimbali za kiuchumi katika shehia hiyo pamoja na mwingiliano wa watu kutoka maeneo tofauti umechangia kwa baadhi ya watoto na vijana kujiingiza katika makundi na tabia hatarishi ambazo zinaweza kuathiri maisha yao na maendeleo ya jamii.

Ametoa wito kwa wananchi kutokaa kimya wanapoona changamoto za watoto na vijana, huku akisisitiza umuhimu wa kuondokana na suala la muhali ili kusaidia kuchukua hatua za mapema.

Kwa upande wao, Sheha wa Shehia ya Mto wa Pwani, Mohammed Ali Ali, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Msingi Mto wa Pwani, Jecha Mohammed Hamza, wamesema wataendelea kushirikiana na wananchi pamoja na taasisi mbalimbali katika kutatua changamoto hizo.

Wamesema hatua mbalimbali zinahitajika ikiwemo kuimarisha malezi ya familia, ufuatiliaji wa watoto, ushirikiano kati ya shule na wazazi, pamoja na kuanzishwa kwa sheria ndogo ndogo za kijiji zitakazosaidia kudhibiti vitendo vinavyoathiri ustawi wa watoto na vijana.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria kikao hicho wamesema miongoni mwa sababu zinazochangia utoro na mporomoko wa maadili ni pamoja na mabadiliko ya malezi ya kileo, muhali na mwingiliano wa watu mbalimbali ndani ya shehia hiyo.

Wameeleza kuwa changamoto hizo zinahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa jamii nzima ili kujenga kizazi chenye nidhamu, uwajibikaji na maadili mema kwa maendeleo ya Shehia ya Mto wa Pwani.