Mwandishi, Nishan khamis, Zanzibar.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe, Cassian Galoss Nyimbo, ameagiza Kamisheni ya Utalii kusitisha ujenzi unaoendelea eneo la Nungwi na kuhakikisha sheria pamoja na taratibu za ujenzi zinafuatwa.Amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika eneo la Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, kwa lengo la kufahamu changamoto zinazojitokeza ndani ya mkoa huo na kuzitafutia ufumbuzi ili kuimarisha amani na usalama.
RC Cassian ,amesema Mkoa wa Kaskazini Unguja umeendelea kuwa eneo muhimu kwa shughuli za utalii na hupokea wageni wengi, hivyo amewataka wawekezaji na jamii kwa ujumla kufuata sheria, kuheshimu mipaka na kuzingatia taratibu za ujenzi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Aidha, ameielekeza Kamisheni ya Utalii kusitisha ujenzi huo na kufanya mazungumzo ya pamoja na Hotel ya Riu kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo baina yao na kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii, Naomi Kassim Mohd, ameomba radhi kwa uongozi wa Mkoa na Wilaya kwa kwenda kinyume na baadhi ya taratibu na sheria za ujenzi zilizopo ndani ya mkoa huo.Ameahidi kusitisha ujenzi huo hadi pale watakapopata ridhaa kutoka kwa mamlaka husika.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mkoa na Wilaya, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa pamoja na watendaji mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.