Mwandishi:Nishan Khamis, Zanzibar.
Wahitimu wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni Zanzibar wametakiwa kutumia ujuzi walioupata kama nyenzo muhimu ya kujenga maisha yao, kujiajiri na kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.Akizungumza katika Mahafali ya 13 ya chuo hicho, Mgeni rasmi Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A, Mheshimiwa Nyange Kher Ali, amesema Serikali ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi inaendelea kuweka msukumo mkubwa katika kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya amali ili kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za ajira.
Amesema elimu ya amali ni msingi wa kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuwapa uwezo wa kuanzisha shughuli zao binafsi. Amewataka vijana kuwa wabunifu, kutumia fursa zilizopo na kuacha utegemezi wa kutegemea ajira pekee, badala yake wawe sehemu ya uzalishaji na maendeleo ya Zanzibar.
Ameeleza kuwa Serikali ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kuweka mazingira bora kwa vijana kupitia mipango mbalimbali ya uwezeshaji, ikiwemo fursa za mikopo isiyo na riba ili kuwawezesha kuanzisha miradi yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA), Dkt. Ali Bakar Silima, amesema ni muhimu kwa walimu na wanafunzi kuendelea kuongeza ubunifu ili kubuni mawazo na miradi inayoweza kutatua changamoto zinazozikabili jamii.
Amesema VTA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha vyuo vinapata vifaa vya kisasa vya mafunzo pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuongeza tija kwa wanafunzi.
Katika risala yao iliyosomwa na Yusuf Mustafa Khamis, wahitimu wameishukuru Serikali ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuwekeza katika vyuo vya amali ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa vijana kupata ujuzi mbalimbali.
Wamesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya kuwasaidia vijana kukabiliana na changamoto za ajira, kupata mwelekeo mzuri wa maisha na kujenga uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa.
Aidha, wameainisha baadhi ya changamoto ikiwemo upungufu wa vifaa vya mafunzo, uhaba wa walimu, mahitaji maalum kwa baadhi ya wanafunzi pamoja na hitaji la kuongeza miundombinu ya vyuo ikiwemo mabweni kwa wanafunzi wanaotoka nje ya Zanzibar.
Wameahidi kutumia elimu waliyoipata kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya Zanzibar kwa ujumla.