Popular services

 Mwandishi, Nishan khamis.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mhe,Idrisa Kitwana Mustafa, leo amefanya ziara maalum katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la kuzungumza na watendaji wa wizara hiyo na kuhimiza utekelezaji bora wa majukumu yao.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kitwana  amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa kisekta, usafi wa mazingira, ukusanyaji wa mapato, ushirikiano na kusaidia juhudi za Rais Dkt Mwinyi katika kuleta maendeleo kwa wananchi. Aidha, ametoa agizo kwa Manispaa ya Kaskazini A na Baraza la Mji kaskazini B kuendeleza  masuala ya usafi ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama wakati wote.

Aidha, amewataka watendaji kuzingatia nidhamu kazini, huku akiwaagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Amesema uzalendo, ulinzi na usalama wa taifa ni mambo ya msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa uadilifu, kuepuka migogoro na vitendo vya rushwa, pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano ili kuhakikisha wizara hiyo na taifa kwa ujumla vinapata maendeleo na huduma bora zaidi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ameir Ali Haji, amesema mkoa huo una jumla ya watumishi 601 amesema fedha zilizo aidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 6.6. katika wizara hiyi ameeleza kuwa fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya watumishi na jamii kwa ujumla, ikiwemo kuimarisha usafi wa mazingira, kutatua migogoro ya ardhi, kukuza shughuli za ujasiriamali na kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji katika mkoa huo.

Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A”, Riziki Daniel Yussuf, amemhakikishia Waziri kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ipasavyo, hususan katika suala la usafi wa mazingira, ili kufikia azma ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuendeleza maendeleo zaidi nchini na kuboresha ustawi wa wananchi.