Popular services

 Mwandishi Nishan Khamis. Zanzibar.

Taasisi ya Sister Island leo imeendeleza utaratibu wake wa kusaidia jamii kwa kutoa msaada wa vyakula na mavazi kwa baadhi ya watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa misaada hiyo ikiwemo mchele,maharage, nguo za watoto na viatu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sister Island, Francesca Michael Jackson, amesema taasisi hiyo itaendelea kusaidia jamii kupitia rasilimali ilizojaaliwa, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza malengo yake ya kusaidia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, hususan makundi yenye mahitaji maalum.
Amesema msaada huo una lengo la kuimarisha ustawi wa jamii na kuwapa faraja pamoja na matumaini watu wenye ulemavu na familia zao. Aidha, ametoa shukrani kwa viongozi wa Wilaya ya Kaskazini A na Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa taasisi hiyo katika utekelezaji wa shughuli zake za kijamii.

Francesca  pia ameahidi kuendelea kushirikiana na jumuiya za watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Kaskazini A na Zanzibar kwa ujumla, ili kuhakikisha wanapata ushirikiano na msaada unaohitajika katika harakati zao za maendeleo.

Kwa upande wao, Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Ali , na Diwani wa Wadi ya Tazari, Twalib Haji Abbas, wameipongeza Taasisi ya Sister Island kwa kuendelea kugusa maisha ya wananchi wenye uhitaji kupitia misaada mbalimbali ya kijamii. Wamesema hatua hiyo inaonesha moyo wa kujali na mshikamano ambao unapaswa kuigwa na wadau wengine wa maendeleo.

Kwa upande wao, wanufaika wa msaada huo wameishukuru Taasisi ya Sister Island kwa kuwakumbuka na kuwapatia msaada wa vyakula na mavazi ambao utawasaidia katika maisha yao ya kila siku. Wamesema msaada huo umeonesha kuwa bado kuna taasisi na watu wenye moyo wa kujali mahitaji ya watu wenye ulemavu, huku wakiiombea taasisi hiyo kuendelea kupata mafanikio ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji.