Popular services

 Mwandishi. Nishan khamis, Zanzibar.

Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A, Mheshimiwa Nyange Kher Ali, amejumuika na madiwani katika mahafali ya saba ya Kituo cha New Rural English Center (NREC) yaliyofanyika Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meya Nyange Kher Ali amewasisitiza vijana na jamii kwa ujumla kutumia fursa ya kujifunza lugha za kigeni ili kuweza kuzifikia fursa za ajira, hususan katika sekta ya utalii ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa pato na ajira nchini.
Amesema Kaskazini Unguja ina fursa nyingi za kiutalii, hivyo ni muhimu kwa vijana kujipanga kitaaluma kwa kujifunza lugha hizo ili waweze kunufaika na fursa zilizopo na kujikwamua kiuchumi.

Aidha, ameipongeza NREC kwa mchango wake katika kuinua elimu ya Kiingereza na ujuzi wa maisha kwa vijana, hatua inayosaidia kuongeza ajira na kuimarisha maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa NREC, Juma Haji Juma, ametoa wito kwa wazazi kushirikiana na walimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo kikamilifu na kupunguza utoro unaoathiri maendeleo ya elimu.

Naye mwakilishi wa wanafunzi, Mwanahawa Haji Haji, amesema kituo hicho kina jumla ya wanafunzi 812, ambapo wavulana ni 322 na wasichana 490, na kimefanikiwa kuhitimu makundi 11 ya mafunzo katika fani mbalimbali, licha ya kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa jengo maalum la kujifunzia na vifaa vya kufundishia.