Mwandishi. Nishan khamis, Zanzibar.
Taasisi ya Salm Turkey Foundation ya Kandwi leo imeadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika Duniani kwa kushirikiana na watoto yatima na wenye mazingira magumu wanaolelewa katika Kituo hicho kilichopo Kijiji cha Kandwi wilaya ya Kaskazini A kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi katika Skuli ya Msingi Kandwi pamoja na kutoa vifaa mbalimbali vya skuli kwa wanafunzi wa skuli hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono maendeleo na ustawi wa watoto.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Taasisi ya Salm Turkey Foundation, Victoria Mwakanjuki John, amesema kuwa kutokana na umuhimu wa siku hiyo wameona kuna haja ya kushiriki katika shughuli zinazolenga kuimarisha mazingira ya watoto ikiwemo kufanya usafi na kutoa vifaa vya masomo na zawadi mbalimbali.
Amesema maadhimisho hayo yanaendana na kauli ya maji safi na vyoo hivyo wameona kuna umuhimu wa kushirikiana na watoto hao katika kuwaelimisha zaidi juu ya umuhimu wa usafi na utunzaji wa mazingira.
Ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana ipasavyo katika malezi ya watoto kwa Maslahi mapana ya taifa bora nchini
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Kandwi, Ame Mwiga Silima, ametoa pongezi za dhati kwa Taasisi ya Salm Turkey Foundation kwa ushiriki wao na msaada walioutoa katika skuli hiyo, akisema ni jambo la muhimu linalosaidia kuongeza hamasa kwa wanafunzi na walimu. Aidha ametoa wito kwa taasisi mbalimbali pamoja na jamii kuendelea kushirikiana kusaidia watoto na sekta ya elimu kwa ujumla.
Nae mlezi wa watoto katika kituo hicho, Asha Twaib Mfaume, amesema zaidi ya watoto 68 wa kike wanaolelewa katika kituo hicho wakiwa ni watoto yatima na wenye mazingira magumu. Ameitaka jamii, wazazi na walezi kuwalea watoto hao katika misingi bora ya maadili ili waweze kufikia malengo yao ya maisha.
Nao watoto wanaolelewa katika kituo hicho wametoa pongezi za dhati kwa Taasisi ya Salm Turkey Foundation kwa malezi bora na huduma nzuri wanazopatiwa, wakisema msaada huo umekuwa chachu ya kuwapa moyo na hamasa katika kutimiza ndoto zao za maisha.
