Popular services

SIKU 16 ZITUMIKE KULETA MABADILIKO MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI WA WANAWAKE NA WATOTO NCHINI-TAMWA-ZNZ

Na,Nishan khamis 

Zanzibar. 

Mjumbe  Wa bodi kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ) Mwatima Issa Rashid, amewataka wanaharakati na jamii kwa ujumla kuzitumia siku 16 za kupinga udhalilishaji kuendelea kuleta  mabadiliko ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto ili kujenga jamii yenye utu, heshima amani na utulivu nchini.

Ametoa wito huo hapo jana  katika maadhimisho ya kupinga siku 16 za vitendo vya udhalilishaji yalioandaliwa na TAMWA Zanzibar, hafla iliyofanyika ukumbi wa Bima, Mperani Mjini Unguja.

Amesea  michango ya wanaharakati na ushirikiano wa wanajamii nafasi kubwa na inathaminika kusaidia mapambano ya vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia ambao wahanga wakubwa wa vitendo hivyo ni wanawake na watoto nchini. 

Aidha amewataka wanaharakati kuitumia siku hiyo kupokea na kujadiliana mchango mbali mbali itakayowasilishwa ili kuwa chanzo cha kujenga ari mpya kuwavutia wengine kuungana nao kupinga vita hivyo.

Amesema kwa sasa TAMWA ina nafasi kubwa ya kupaisha sauti za wanawake na makundi mengine kwa kua mstari wa mbele kushajihisha na kutoa taaluma kupitia vyombo vya habari ili kufikia jamii kubwa na kwa wakati.

Alifahamisha kuwa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinafanya jitihada mbali mbali kupinga vitendo vya udhalilishaji ni vyema wanaharakati kuendelea kuungana bila ya kuchoka kupinga vitendo hivyo.


Mwatima amesema lengo la maadhimisho hayo ni kujenga jamii iliyohuru kuepukana na vitendo vya udhalilishaji na majanga mengine yanayochafua sifa na maadili yanayochafua maisha ya kila binaadamu.

Awali akiwasilisha ripoti katika hafla hiyo Afisa Programu kutoka Mradi wa Michezo kwa Maendeleo (GIZ) Khairat Haji alisema kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, kutoka Januari hadi Oktoba 2024 jumla ya matukio ya udhalilishaji yaliotokea na kuripotiwa ni 1582 huku waathirika ni 1583.


Alisema kati ya idadi hiyo 1337 ni watoto ambapo wasichana ni 1095 na wavulana ni 242 ambao ni sawa na asilimia 84.4 ya waathirika wote.

Alieleza kuwa watoto wenye umri wa miaka 15 hadi 17 ni 693 ni sawa asilimia 52, ambapo wanawake watu wazima walioathirika 183 na wanaume watu wazima 63, huku wilaya ya Magharibi B ikiongoza kwa matukio ya udhalilishaji 386, ikifuatiwa na Mjini 344 na 373 magaharibi A.

Baadhi ya wanaharakati waliohudhuria maadhimisho hayo, wamesema miongoni mwa mambo yanayo weza kupunguza vitendo vya udhalilishaji nini wazazi kuswahirikisha watoto katika michezo kwani michezo inamfanya mtu kuwa na kujiamini pamoja kuimarisha afya mwilini. 

Baadhi ya wazazi na viongozi wa dini waliohudhuria wamesema miongoni mwa mambo yanayopelekea kuwepo kwa vitendo hivyo ni upungufu wa imani,malezi ya mzazi mmoja pamoja na muhali ni mambo yanayo sababisha kuendelea kuwepo,hivyo wameziomba taasisi na serikali kuendelea kushirikiana ipasavyo katika kupambana na vitendo hivyo. 

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni "kuelekea 2030 tuungane kutafakari na kuchukua hatua kumaliza udhalilishaji dhidi ya wanawake Zanzibar".