Popular services

RAIS MWINYI:ZANZIBAR IPO TAYARI KWA MASHINDANO YA CHAN 2025


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi amelihakikishia Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF kuwa Zanzibar ipo tayari na inajiandaa  vema kufanikisha Mashindano ya CHAN yanayotarajiwa kufanyika Februari mwakani. 


Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 19 Disemba  2024 alipozungumza na Rais  wa  Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF)  Patrice Motsepe aliefika Ikulu Zanzibar .

Aidha , Rais Dk. Mwinyi  ameeleza kuwa  Serikali inaendelea na Ujenzi wa Miundombinu ya Viwanja kwa kasi kubwa ili ikamilike kwa wakati  na kufanikisha Mashindani hayo na kuishukuru CAF kwa Kuiamini Zanzibar.


Rais Dk.Mwinyi amesisitiza kuwa mbali na viwanja pia Serikali  inajiandaa  na kuwa na  hoteli bora  na za kutosha  zitakazokuwa na uwezo wa kupokea  wageni watakaofika  kwa ajili ya mashindano hayo na huduma bora.

Naye, Rais wa CAF  Patrice Motsepe ameeleza kufarijika  na  maandalizi  ya Kiwanja cha New Amani Complex na utayari wa Zanzibar  kufanikisha mashindano hayo.

Halikadhalika Rais Motsepe amesifu juhudi zinazoendelea za kuimarisha viwanja vya ndege , miundombinu  ya  barabara na ongezeko la hoteli  mambo aliyosema kuwa ni muhimu katika kufanikisha Mashindano.