Popular services

MATUKIO 136 YA UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA YAMERIPOTIWA MWEZI NOVEMBA, 2024


Kwa mujibu wa ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar Jumla ya matukio 136 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwezi wa Novemba, 2024 ambapo waathirika walikuwa 136. Waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 86.0, wanawake asilimia 9.6 na wanaume asilimia 4.4.

Idadi ya matukio kwa mwezi yamepungua kwa asilimia 7.5 kufikia matukio 136 mwezi wa Novemba, 2024 kutoka matukio 147 kwa mwezi wa Oktoba 2024. Aidha, matukio ya kuingilia kinyume na maumbile na shambulio la aibu/kukashifu yameripotiwa kuongezeka  kwa mwezi wa Novemba 2024.

Idadi ya matukio kwa mwaka yamepungua kwa asilimia 20.9  kufikia matukio 136 kwa mwezi Novemba, 2024 kutoka matukio 172 kwa mwezi wa Novemba, 2023. Matukio ya  kuingilia kinyume na maumbile na shambulio la aibu/kukashifu yameripotiwa kuongezeka  kwa mwezi Novemba, 2024. 

Wilaya ya Magharibi “A” imeripotiwa kuwa na matukio mengi ukilinganisha na wilaya nyengine (matukio 39) sawa na asilimia 28.7  ikifuatia wilaya ya Magharibi “B” ambapo yameripotiwa matukio 32 (asilimia 23.5).

Wilaya ya Micheweni na Mkoani zimeripotiwa kuwa na idadi ndogo ya matukio, matukio mawili (2) sawa na asilimia 1.5 kwa kila Wilaya .

Wilaya ya Magharibi “B” imeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya kubaka ikilinganishwa na Wilaya nyengine, ambapo jumla ya matukio ya kubaka 15 sawa na asilimia 28.8 kati ya matukio yote ya kubaka yaloripotiwa.


Kati ya matukio 52 ya kubaka yalioripotiwa kwa mwezi wa Novemba, 2024, matukio matano (5) sawa na asilimia 38.5 yameripotiwa kwa wanawake na matukio 47 yameripotiwa kwa wasichana sawa na asilimia 90.4.