Popular services

*TUSHIRIKIANE KUTATUA CHANGAMOTO ZA VIJANA ZANZIBAR*

 Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan amesema  Baraza la Vijana Zanzibar lipo tayari  kushirikiana na Taasisi binafsi zinazoshughulika na masuala ya Vijana kwa lengo la kuwasaidia  Vijana wa kizanzibari kufikia malengo yao .


Ameyasema hayo huko ofisi ya Taasisi ya ZAFAYCO Mombasa kwa Mchina alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo  inayoshughulika na masuala mbalimbali yanayowahusu Vijana. 


Amesema ipo haja kwa Taasisi zisizo za Kiserekali kufanya kazi kwa karibu na Baraza la Vijana Zanzibar kutokana na mabaraza ya Vijana kuwepo shehia zote 388  za  Zanzibar . 


Akizungumzia lengo la Taasisi ya Baraza la Vijana Zanzibar  ni kuwasaidia Vijana kufikia ndoto  zao bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, dini au Kabila.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ZAFAYCO Abdullah Abeid  amesema kupitia Taasisi anayoiongoza itashirikiana na Baraza la Vijana Zanzibar kuhakikisha wanamfikia kila kijana wa kizanzibari anapata huduma zinazotolewa na Taasisi hizo.


Akizungumzia  huduma wanazozitoa katika Taasisi  hiyo ni pamoja na masuala  ya uchumi,  siasa ,  afya na elimu.