KWA MUJIBU WA OFISI YA MTAKWIMU MKUU ZANZIBAR JUMLA YA MATUKIO 148 YA UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA YAMERIPOTIWA KWA MWEZI SEPTEMBA, 2024
Jumla ya matukio 148 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwezi wa Septemba, 2024 ambapo waathirika walikuwa 148. Waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 87.9, wanawake asilimia 7.4 na wanaume asilimia 4.7.
Idadi ya matukio kwa mwezi yamepungua kwa asilimia 5.7 kufikia matukio 148 mwezi wa Septemba, 2024 kutoka matukio 157 kwa mwezi wa Agosti, 2024. Matukio ya shambulio, shambulio la aibu/Kukashifu na kulawiti/kunajisi yameripotiwa kuongezeka kwa mwezi wa Septemba 2024. Matukio ya kutorosha na Shambulio yameripotiwa kupungua kwa mwezi Septemba, 2024.
Wilaya ya Magharibi “A” imeripotiwa kuwa na matukio mengi ukilinganisha na Wilaya nyengine (matukio 41) sawa na asilimia 27.7 ikifuatia Wilaya ya Magharibi “B” ambapo yameripotiwa matukio 37 (asilimia 25.0).
Wilaya ya Wete, Micheweni na Mkoani zimeripotiwa kuwa na idadi ndogo ya matukio, matukio matatu (3) yameripotiwa kwa kila Wilaya sawa na asilimia 2.0.
Wilaya ya Magharibi “B” imeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya kubaka ikilinganishwa na Wilaya nyengine, ambapo jumla ya matukio ya kubaka 17 sawa na asilimia 26.6 kati ya matukio yote ya kubaka yaloripotiwa.
Kati ya matukio 64 ya kubaka yalioripotiwa kwa mwezi wa Septemba, 2024, matukio mawili (2) sawa na asilimia 3.1 yameripotiwa kwa wanawake na matukio 62 yameripotiwa kwa wasichana sawa na asilimia 96.9.
